Mistari kizazi kipya cha michano

MIAKA ya nyuma gemu ya hiphop kibongo bongo ilitawaliwa na mastaa kama Sugu, Balozi Dolasoul, Solo Thang, Prof Jay, Juma Nature, Jay Moe, Afande Sele na wengine wengi.

Baada ya kuondoka kizazi hiki kikaingia kizazi cha kina Fid Q, Roma, Joh Makini na wengine wengi ambao walifanya muziki wa Hip Hop kuendelea kupendwa na wale ambao wanaamini katika muziki huo.

Wakati kizazi hicho kikiwa kinaendelea, katikati wakaingia Young Dee, Country Boy, Stamina, Dogo Janja, Young Killer na wengineo.

Kama ambavyo waliondoka walioanzisha michano hii kibongo bongo basi kwa sasa wapo vijana ambao wapo katika muziki huu na michano yao sio ya kitoto kwani wamegeuka kuwa lulu katika gemu hii kutokana na mashairi yao.

Licha ya uwepo wao tu, mpaka sasa wamekuwa na ushindani mkubwa wa kuachia ngoma kali ambazo sasa zinakuwa kama vile zinaanza kuwaweka njia panda mashabiki wasijue waegemee upande upi kutokana na ubora wa kila msanii.

Mwanaspoti linakuletea madogo ambao muenendo wao unaonyesha dhahiri kwamba wanarithi mikoba ya kaka zao ambao wamepishana katika muziki wa Hip Hop ya Bongo.

CON BOI                                                            

Miondoko yake sio ya kibongo bongo hata kidogo ni taipu ya wale wasanii wa Marekani ambao wanakuwa wanachana sana kuhusu maisha ya uhalisia huku wakiwa na muonekano wa tofauti.

Con Boi pia hata muonekano wake alivyoutengeneza ni wa kisanii wa mbele mbele kutokana na kuchora kwake Tattoo mwili mzima na kufanania na msanii wa Marekani, Lil Wayne.

Pia kasi yake ya kutamba hivi sasa imezidi kuwa kubwa kwenye soko la Hip Hop nchini akikimbizana na vijana wenzake huku akiwa ameachia ngoma ya Till I Die ambayo imeungwa mkono mpaka na msanii wa Marekani Fat Joe baada ya kujibu.

YOUNG LUNYA

Huyu mwana ni kati ya watu wabaya zaidi katika michano. Young Lunya, ni msanii ambaye anatumia mashairi yake kusifia, kufurahisha na hata kufunza pia.

Lunya pia anasifika kwa staili ya kuchana mistari ya kujibizana (Free Style) kama ile ya Announcement ambayo imekuwa ni kivutio kikubwa kwa mashabiki ambao wanamfuatilia msanii huyu.

Staa huyu wa kizazi cha sasa anasifika pia kwa kuandikia wasanii wenzake mistari, nyimbo mbalimbali ambazo zinafanya vizuri mpaka sasa na yeye akiendelea na maisha mengine.

NACHA

Baada ya uwepo wa Mrisho Mpoto kufikisha mashairi huku akiwa anaongea, jambo hilo limegeuka upande wa Hip Hop kupitia kwa msanii huyu ambaye anatamba kwa mashairi yake akichana huku akiwa haimbi bali anazungumza.

Moja ya nyimbo zake ambazo zinatamba kwa sasa ni Darasa Huru. Moja ya mistari ambayo ameimba humo “Tatizo ni kwamba hatuelewi bali tunakariri, yani hatuna utofauti na wanaoamini kumuabudu Mungu ni Ijumaa na Jumapili utakwenda peke yako kaburini ukakae, swali kabla hujasaliwa.”

Nyimbo zake zimekuwa zikitoa ujumbe kwa jamii hali ambayo katika mtandao wa YouTube amejiwekea uhakika wa kupata watazamaji wengi kwani anapotoa ngoma inaenda sambamba na video.

MAARIFA ‘THE BIG

THINKER’

Mwenyewe anajiita Kibaha Finest, anawakilisha sehemu anayotokea lakini amejikuta akipata mashabiki kutoka katika kila pembe ya Tanzania kutokana na aina ya muziki ambao anaufanya.

Alianza kwa kufanya ngoma yeye mwenyewe lakini baadaye akawa anaonekana katika kituo cha redio akiwa anafanya mitindo huru (Free Style) na baada ya hapo akachukuliwa na rais wa Manzese, Madee.

Akiwa anapigwa tafu na Madee ameweza kufanya ngoma zenye ubora wa juu na Barnaba ‘Ukiniacha’ na nyingine aliyomshirikisha Dogo Janja ambayo inakwenda kwa jina la Acha Iwe.

RAPCHA

Mwenyewe anajiita ni King of 90’s, yani kwa vijana ambao wamezaliwa miaka ya kuanzia 90 yeye ndio baba yao kwenye utunzi wa mashairi na mpaka sasa bado anapambana kuonyesha kwamba yupo kwenye njia sahihi.

Prodyuza P Funk Majani kwa muda mrefu alisimama kufanya kazi ya kutengeneza ngoma, lakini kwa dogo huyu aliamua kusimamia shoo yeye mwenyewe na kufanya nae ngoma nyingi.

Kwasasa Rapcha anatamba na ngoma ‘Amen’ ambayo amemshirikisha mkongwe Lady Jaydee ambayo ameelezea namna ambavyo anashukuru Mungu anavyozidi kumbariki kila siku kama ambavyo anasema “Niwapo kwenye njaa nikumbushe kwamba ndege hawalimi ila hawawezi kosa chochote, nisitamani magari nisiyoweza kuyaendesha.”