Mh!corona imepiga teke dili zao

Friday March 20 2020

uzinduzi wa albam yake ya ‘Afro East’ , Konde Boy ,ukumbi wa Mlimani City, bonge shoo ,virusi vya corona,MwanaFA akutwa na corona,Mwanasport,

 

By Rhobi Chacha

MIONGONI mwa watu wanaoweza kujiita ni wenye bahati ni mwanamuziki Harmonize. Aliandaa uzinduzi wa albam yake ya ‘Afro East’ kwa gharama kubwa na ukafana. Mitandao ya kijamii ikatawaliwa na stori zake. Kila mtu alizungumzia namna Konde Boy alivyofunika kwa bonge shoo kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam wikiendi iliyopita.

Hata bosi wake wa zamani, Diamond Platnumz akaonyesha kuukubali mziki mnene wa Konde Boy na akaomba watu wamsapoti kununua kazi zake.

Lakini hebu fikiria kama katazo hili la kufanyika kwa maonyesho lililotolewa na serikali katika kupambana na kusambaa kwa mlipuko wa virusi vya Corona lingetolewa siku moja kabla ya onyesho. Konde angekuwa katika hali gani?

Wakati dunia sasa inapambana na kusambaa kwa virusi vya Corona, Tanzania pia imejumuika kwa kusimamisha kwa muda wa mwezi mzima shughuli zote zinazohusu mikusanyiko kama michezo, burudani, masomo na mikutano ya kisiasa kupitia tamko lililotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Machi 17.

Haya hapa ni baadhi ya matamasha yaliyokumbana na fagio la Corona.

Diamond - Shoo za Ulaya

Advertisement

Supastaa wa Bongofleva, Diamond Platnumz anajulikana kwa kuwa na shoo nyingi za nje ya Tanzania kuliko anazofanya ndani ya taifa hili.

Haya ni maonyesho ambayo yanamuingizia Mondi mkwanja mrefu.

Lakini katazo la dunia la kufanyika kwa mikusanyiko, limepiga ‘stop’ dili kibao za staa huyu wa ngoma kali ya ‘Jeje’.

Kiufupi, kabla ya kutangazwa kwa katazo hili, Mondi alikuwa ana ratiba ndefu ya kutumbuiza katika nchi mbalimbali za Ulaya.

Miongoni mwa ratiba zake zilizovurugika ni ile ya Finland Machi 14, Ujerumani Machi 28, Ufaransa Aprili 3 na Sweden Aprili 4.

Meja Kunta - Dili la India

Achana na utamu wa wimbo wake wa ‘Mamu’ uliompa shavu la kwenda kufanya shoo nje ya nchi kwa mara ya kwanza. Wimbo wake mpya wa ‘Wanga (Wabay)’ alioshirikiana na Lavalava, umevuma hadi nje ya mipaka ya Tanzania na baadhi ya wasanii wa Marekani kama Alicia Keys, mke wa mwanamuziki na produza, Swizz Beatz alijirekodi akicheza wimbo huo na kuzidisha kuupa shavu.

Mkali huyu wa ‘singeli’ aliyezidisha umaarufu wake baada ya yeye na timu yake kutengeneza kiki kwamba amefariki dunia ajalini Segera, mkoani Tanga, alikuwa aende kutumbuiza kwenye shoo ya India Aprili 10 kabla ya zuio hilo lililotoka kwa serikali.

Rayvanny

Shoo za nje ya nchi kwake ni jambo la kawaida kama ilivyo kwa bosi wake Diamond Platnumz na amekuwa akipata dili nyingi za pesa.

Safari hii alikuwa aende kupiga shoo yake Kenya Aprili 11 akitamba na ngoma zake kali kama ‘Tetema’, ‘Chuchumaa’, ‘Natafuta kiki’ ‘Kwetu’ na nyingine nyingi.

Rayvanny kama ilivyo kwa Diamond na Meja Kunta inamlazimu aahirishe shoo yake hiyo kutokana na serikali za nchi zote mbili kupiga marufuku mikusanyiko ya watu zikiwemo shoo za burudani.

Muumini Mwinjuma

Unaweza ukasema amerudi kwa kasi kwani tangu aachie kibao chake kipya cha ‘Nimefulia’ akiwa na bendi mpya ya Shadai.

Jamaa alikuwa amepata dili la kwenda kufanya shoo mkoani Dodoma katika Ukumbi wa Platnum 4G ikiwa ni uzinduzi wa bendi hiyo.

Uzinduzi huo ambao ulikuwa ufanyike Machi 28 lakini kutokana na zuio la serikali katika vita kupambana na kusambaa kwa virusi vya ugonjwa wa Corona, uzinduzi huo umeahirishwa hadi itakapotangazwa tena.

Msanii huyu mkongwe wa muziki wa dansi amewahi kutamba na nyimbo kama ‘Tunda’, ‘Maisha Kitendawili’, ‘Mgumba’ na nyingine nyingi zilizompa jina kwenye tasnia hii ya muziki wa dansi kabla ya kuwa kimya kwa muda na sasa amerudi kivingine.

Muumin, Mondi, Meja Kunta na Rayvanny ni miongoni tu mwa wasanii ambao kipindi hiki kigumu kimekatisha dili zao za kupiga pesa.

Advertisement