Mbosso aeleza uhusiano wake na marehemu Martha

Thursday September 12 2019

 

By Elizabeth Edward

Dar es Salaam. Wakati mitandaoni watu wakihoji uhusiano wa mchekeshaji Martha (marehemu) na msanii wa WCB, Mbosso kufahamika baada ya kifo cha msichana huyo, ukweli umewekwa wazi.

Jana Jumatano Septemba 11, 2019 baada ya taarifa za kifo, Mbosso aliandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa Instagram akionyesha ni kwa namna gani ameguswa na msiba huo.

Maneno hayo yalizua mjadala mpya inakuwaje yanazungumzwa baada ya Martha kufariki dunia.

Mbosso amevunja ukimya na kueleza kuwa aliwahi kuwa kwenye uhusiano na Martha na kupata mtoto wa kiume ila mchekeshaji huyo hakutaka suala hilo kuwa wazi kwa sababu za familia.

Amesema licha ya kuwa wao walipendana, familia ya mchekeshaji huyo haikupenda Mbosso kuwa na Martha.

“Martha nilikuwa naye karibu kuanzia urafiki hadi kwenye uhusiano na kufikia kupata mtoto ambaye ana miaka minne sasa lakini inaonekana familia yake haikuridhishwa na mimi,”

Advertisement

“Tulipambana lakini mwisho wa siku tukaamua kila mtu aendelee na maisha yake na yeye akaniomba tusiwe tunazungumzia kuhusu uhusiano wetu wala mtoto tuliyempata,” amesema Mbosso

Amesema mwanzoni alipata shida kukubaliana na ombi hilo lakini baadaye alielewa na wote wakawa wanakana kuhusu uhusiano wao kila walipoulizwa.

Amesema licha ya kuachana waliendelea kuwa marafiki na kuwasiliana kwa ajili ya mtoto.

“Niliwasiliana naye akaniambia anataka kuhama Sinza na akanitumia picha za nyumba lengo lilikuwa amchukue mtoto ambaye yuko Tabora kwa sasa, wahamie nyumba mpya,”

“Mara ya mwisho aliniambia kichwa kinamuuma nikajua ni malaria au uchovu sikujua kama ndio kingechukua uhai wake,” amesema Mbosso.

Advertisement