Marioo kutoka kwa Mama Ntilie hadi studio

Friday October 11 2019

 

By Rhobi Chacha

MIONGONI mwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya walioliteka anga la Bongofleva huyu hapa ni Marioo.

Washa TV yako, sikiliza redio ya FM au tembelea kurasa za mitandao ya kijamii, kote huko utakutana na kazi ya Marioo.

Kipaji, uchapakazi na kutokata tamaa, ni kati ya mambo yanayomfanya kijana huyu kutokea katika maisha ya chini awe gumzo kwenye gemu ya kizazi kipya akipiga pesa freshi kabisa.

Kazi za mikono yake zilimtangulia kuwa maarufu baada ya kuwaandikia wasanii tele ngoma kali zilizotamba. Na sasa ni zamu yake kubamba.

ALIKOTOKEA

Marioo ambaye jina lake kamili ni Omari Mwanga alizaliwa mwaka 1995 jijini Dar es Salaam na akiwa bado mtoto mdogo, wazazi wake walimpeleka kuishi kwa bibi yake, Rufiji mkoani Pwani.

Advertisement

Baada ya kumaliza elimu ya msingi na kushindwa kuendelea na elimu ya sekondari, alilazimika kufanya kazi katika mgahawa (mama ntilie) na ndipo alipoamua pia kujihusisha na muziki.

“Napambana sana kwenye muziki kwani kabla ya hapa nilishawahi kufanya kazi za kwa mama ntilie mgahawani,” anasema Marioo ambaye ni Mndengereko kutoka Rufiji, Pwani lakini amezaliwa Temeke, Dar es Salaam.

“Katika kipindi ambacho nimeanza kujitambua mama alinipeleka kwa bibi yangu Kibiti, huko nikasoma shule ya msingi na sekondari na nikaishia kidato cha kwanza kutokana na sababu mbalimbali za maisha.

“Kwetu tupo watoto watatu, mimi ni wa mwisho. Baba yangu alikuwa kondakta na alishafariki dunia. Mama yangu yupo, naye alikuwa anafanya kazi kiwandani huko Vingunguti,” anasema Marioo.

KUJIINGIZA KWENYE MUZIKI

Marioo anafahamika kwa ngoma zake kali kama ‘Dar Kugumu’, ‘Manyaku’, ‘Ifunanya’, ‘Inatosha’, ‘Raha’, ‘Chibonge’ alioshirikishwa na Abbah Process na wimbo mpya alioshirikishwa hivi karibuni wa ‘Weka’ wa msanii nguli nchini, Dully Sykes.

Anasema kuingia kwake kwenye muziki kulitokana na kushindwa kuendelea na elimu ya sekondari kutokana na changamoto za kifamilia.

KWA NINI MARIOO?

Anasema jina Mario (linatamkwa Marioo) limetokana na jina lake halisi ya Omari, akiitoa herufi ya kwanza “O” na kuipeleka mwisho wa jina.

Na anasisitiza Marioo yake si ile inayotumiwa kimjini mjini ikimaanisha vijana wa kiume wanaopenda ganda la ndizi (kuteleza) katika maisha ya mteremko ya kulelewa na wanawake wenye vipato vikubwa.

AJIUNGA THT

Anasema baada ya mapambano ya muda mrefu katika muziki alipata bahati ya kujiunga na kituo cha kuendeleza vipaji vya muziki cha Tanzania House of Talent (THT), ambacho kilikuwa kinamilikiwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Uzalishaji na Vipindi wa Clouds Media, Ruge Mutahaba.

Anasema huko alikutana na wasanii ambao tayari walitoka kimuziki na kufanya kazi nao, ikiwamo kuwatungia nyimbo.

UANDISHI WA NYIMBO

Mbali na kuimba, Mariaoo ni mwandishi wa nyimbo za wasanii na ameandika baadhi ya ngoma kali zilizotamba kama ‘Banana’ ya Janjaro, ‘Nampa Papa’ ya Gigy Money, ‘Wasikudanganye’ ya Nandy, ‘Nabembea’ ya Ditto, ‘Pambe ya Christian’ Bella, ‘Mchakamchaka’ ya Shilole, ‘Bado’ ya Mwasiti na Billinas na nyingine.

Anasema hachagui aina ya nyimbo, anatumia beats na mizuka ya beat ndiyo anaandika ngoma.

Baada ya kuwaandikia nyuma ya pazia wasanii kadhaa nyimbo zilizotamba huku yeye akiwa hafahamiki, hatimaye akaamua ajitose kuimba. Na hakika ulikuwa ni uamuzi sahihi, kwani tangu hapo amebaki kuwa juu. Anapiga pesa.

Hata hivyo, kati ya vitu anavyofurahia ni kufanya kazi na Dully Sykes kwani alikuwa anamfuatilia tangu siku nyingi katika muziki wake na ndiye aliyemsaidia kufika hapa.

“Nakumbuka niliwahi kumsikilizisha kazi zangu kipindi cha nyuma na kuniahidi kunisaidia, nikakaa naye kwenye studio yake pia alinisaidia kama Sh500,000 niongezee kwenye kutengeneza video.”

AZUSHIWA YA ASLAY

Hata hivyo, kutokana na kutoa nyimbo mfululizo, Marioo amekanusha habari za baadhi ya watu wanaodai ataishia kupotea kama ilivyotokea kwa msanii Aslay ambaye aliachia nyimbo mfululizo hadi kuishia njiani.

Hata hivyo, Aslay mwenyewe aliibuka na kudai aliibiwa daftari lake la nyimbo na baada ya kulipata ndipo aliamua kutoa mfululizo na baada ya kuisha sasa anatoa kwa wakati.

CHIBONGE UMEMPA HESHIMA

Anasema ngoma ya ‘Chibonge’ ambayo ameshirikishwa na Abbah Process imempa heshima ambayo hakuwahi kufikiria kama ataipata katika tasnia ya muziki.

“Kikubwa ambacho najivunia katika ngoma ya ‘Chibonge’ ni heshima niliyoipata. Wengi wamegundua uwezo wangu katika kuimba kupitia wimbo huu,” anasema Marioo.

Anasema ameweza kufanya vizuri kwenye muziki wake kutokana na nidhamu na ndio pia iliyomwezesha kufanya video bure kutoka kwa mtayarishaji Adam Juma ya wimbo wake wa kwanza wa ‘Dar Kugumu’.

ALIVYOKUTANA NA ABBAH

“Nilikuwa nimemsindikiza mshkaji wangu mmoja kwenda kurekodi nyimbo zake. Katika mazingira hayo ya studio nikakutana na jamaa mmoja anaitwa Tunchi Master ambaye aliniambia huwa wanarekodi kwa Sh300,000 ila akaniambia nilipe nusu. Nikajichanga nikalipa nikafanya wimbo ila tatizo likawa kwenye ‘mixing’, alinizungusha sana,” anasema.

“Kuna siku Abbah aliusikia wimbo wangu akaupenda, akakubali kunifanyia ‘mixing’ na kuanzia hapo akaniambia niwe msanii wake, tukawa tunafanya kazi na ndio hivyo tukatoa wimbo wa ‘Chibonge’ na namshukuru sana kwani amenifanya kuwa msanii mkubwa sasa.”

KULIPISHA WASANII

Anasema kutokana na sasa kuingia kwenye kuimba na yupo chini ya Hanscana, anapowaandikia wasanii nyimbo zake huwatoza kuanzia Sh1 milioni.

“Kwa sasa siwezi kufanya kazi kwa ajili ya kujulikana, niliowapatia wanatosha, mtu anayehitaji wimbo ajipange kifedha ama tuandikishiane mkataba kwa ajili ya mapato yatakayopatikana kutokana na wimbo huo na sasa nawatoza Sh1 milioni,” anasema.

“Mimi nimeanza kufanya sanaa chini kwa chini kwa muda mrefu, hivyo watu wasistushwe na mafaniko wanayoyaona leo, yametokana na muziki na hakuna kingine,” anasema Marioo.

MAPENZI

Marioo aliwahi kuhusishwa kutoka kimapenzi na mwanadada Amber Lulu ambaye pia ni msanii wa Bongo Fleva. Hata hivyo, mwenyewe amekana,

“Sijawahi kuwa na uhusiano na Amber Lulu, mimi namchukulia kama dada yangu na si yeye tu, hakuna msanii niliyewahi kutoka naye,” anasema.

Anasema ukaribu wake na Amber Lulu ulitokana na shughuli zao za muziki lakini si kitu kingine. Anasema hana mpenzi na hafikirii kuwa naye kwa sasa.

“Nimejiwekea malengo katika muziki ambayo nimeanza kuyatimiza, hivyo sitaingia katika ulimwengu wa mapenzi mpaka sanaa itakaponilipa,” anasema Marioo.

Advertisement