Mademu wa wanamichezo mastaa wanavyopiga pesa ndefu Insta

Muktasari:

Mwimbaji huyo wa wimbo wa Hips Don’t Lie amekuwa na mafanikio kuliko mumewe, beki wa Barcelona, Pique kwa sababu anamiliki mara nne ya wafuasi kwenye Instagram wanaomfuata kipenzi chake huyo, anayewahi kukipiga pia kwenye kikosi cha Manchester United.

LONDON, ENGLAND . KIMWANA wa beki wa mpira, Gerard Pique, mwimbaji wa pop, mrembo Shakira amewapiga bao Victoria Beckham na Gisele kwenye orodha ya wake wa wanamichezo mastaa wanaopiga pesa ndefu kupitia mitandao ya kijamii.

Wakikusanya wafuasi wengi kwenye mtandao wa Instagram wanawake hao wamelitumia jambo hilo kama fursa muhimu ya kupiga pesa za kutosha na hivyo kuongeza kipato kwenye familia zao.

Kitu kisichoshangaza ni mrembo wa muziki wa kutoka Colombia, Shakira ameibuka namba moja kwa mujibu wa Golf Support na Influencer Marketing Hub.

Mwimbaji huyo wa wimbo wa Hips Don’t Lie amekuwa na mafanikio kuliko mumewe, beki wa Barcelona, Pique kwa sababu anamiliki mara nne ya wafuasi kwenye Instagram wanaomfuata kipenzi chake huyo, anayewahi kukipiga pia kwenye kikosi cha Manchester United.

Kinachoripotiwa ni, kila posti ya tangazo anayoposti Shakira kwenye ukurasa wake wa Insta gaharama yake ni Pauni 123,355.

Kwenye hilo amemwacha kwa mbali sana, mwimbaji wa zamani wa kundi la Spice Girl, mfanyabiashara na mbunifu wa mitindo, mrembo Victoria, ambaye ni mke wa mwanasoka wa zamani David Beckham.

Victoria ana wafuasi 27.3 milioni kwenye ukurasa wake huo wa Instagram na ameripotiwa kutoza Pauni 55,991 kwa kila posti ya tangazo anayoweka kwenye ukurasa wake huo.

Mara nyingi, ukurasa wake hio, Victoria amekuwa akiweka picha za familia yake na hivyo karibuni alijiweka akiwa na Kourtney na Kim Kardashian, posti iliyopata ‘like’ kibao.

Lakini, kwenye kuvuna mapato kupitia mitandao ya kijamii, David Beckham amekuwa akifanya vizuri zaidi kuliko mke wake licha ya kwamba amestaafu soka siku nyingi na sasa anapiga pesa kwa kutumia jina lake tu ambalo alilitengeneza wakati huo akiwa Man United na Real Madrid.

Mwanamitindo wa Kibrazili, Gisele Bundchen anashika namba tatu. Mrembo Huyo mwenye umri wa miaka 39, ambaye ni mke wa staa wa mchezo wa NFL, Tom Brady ana wafuasi 15.5 milioni kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Posti yoyote ya tangazo inayotokea kwenye ukurasa wa Bundchen, moja ya wanamitindo maarufu zaidi duniani, imeripotiwa kugharimu Pauni 31,819.

Mrembo La La Anthony, mke wa staa wa NBA, Carmelo Anthony yupo kwenye namba nne. Mwanamke huyo aliyepata umaarufu mkubwa kwenye MTV, posti ya tangazo lolote inayotokea kwenye ukurasa wake basi inagharimu Pauni 20,009.

Kwenye namba tano yupo mshindi wa American Idol wa mwaka 2005, mrembo Carrie Underwood, ambaye ni mke wa staa wa mchezo wa Ice Hockey, Mike Fisher.

Carrie Underwood amemzidi kwa kiwango kikubwa sana namba ya wafuasi kwenye ukurasa wake wa Instagram, huku posti yoyote ya tangazo inayotokea kwenye ukurasa wake huo kuwagharimu wenye tangazo lao kumlipa Pauni 18,910.

Mwigizaji na mtangazaji wa televisheni, mrembo Kristin Cavallari, aliyeolewa na staa wa NFL, Jay Cutler na yake pia si hapa, mrembo huo amekuwa akiwachaji watu wanaotaka kuweka matangazo yao kwenye ukurasa wake, Pauni 7,770 kwa kila posti.

Kwenye namba sana yupo mwimbaji mwingine wa muziki wa Country, mke wa Eric Ducker, mrembo Jessie James Decker.

Wawili hao walifunga ndoa mwaka 2013 wakati huo Eric alikuwa akicheza Denver Broncos, huku Jessie, 31, kwenye ukurasa wake wa Insta kila posti ya tangazo anayoweka huko basi amewatoza wenye tangazo lao Pauni 6,522.

Mke wa kipa, Iker Casillas, mrembo Sara Carbonero mambo yake nayo si mabaya kwenye kutumia ukurasa wake wa Insta kupiga pesa nyingi, ambapo amekuwa na wafuasi 2.6 milioni, kila posti ya tangazo anayoweka kwenye ukurasa wake basi gharama yake ni Pauni 5,326.

Wanaokamilisha kwenye 10 bora ya wanawake wa wanamichezo maarufu wanaopiga pesa nyingi kupitia mtandao wa kijamii wa Insta ni wake wa wachezaji maarufu maarufu wa mpira wa kikapu huko Marekani.

Wawili hao ni mke wa Kobe Bryant, mrembo Vanessa na mke wa Lebron James, mrembo Savannah, ambao kwenye kurasa zao za Insta, kila tangazo linalotokea huko basi wamelipwa Pauni 2,914 na Pauni 2,619 mtawalia.