Kuna sehemu Bongo Movie wamekosea

Sunday July 19 2020

 

By BADRU KIMWAGA

WIKIENDI iliyopita ilikuwa tamu sana kwa wana Msimbazi. Ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Yanga na kuwazuia watani wao waikose tiketi ya kimataifa mwakani, kwani ilikuwa jambo kubwa kuliko hata Ubingwa wa Ligi Kuu Bara walioupata kwa msimu wa tatu mfululizo. Ndivyo Simba na Yanga zilivyo. Kama niliovyotabiri kwamba Bernard Morrison hata kuwa na maajabu ndivyo ilivyokuwa.

Jamaa aligeuka kituko, ila nikiri na kuwapa pongezi waamuzi waliolichezesha ambao awali nilikuwa nina wasiwasi nao kutokana na kutokuwa na uzoefu wa mechi za Kariakoo derby. Kama wataendelea kuchezesha walivyocheza pambano lile la Jumapili, kwa umri walionao ni wazi watafika mbali.

Kwa hakika Kariakoo derby lilikuwa pambano tamu na lililodhibitisha tofauti na mchele na chuya. Uwanja wa Taifa kuliko na tofauti kubwa ya Simba na Yanga ukiachana na zile blabla za mitaani.

Simba walikuwa bora na walistahili ushindi ule. Yanga ni kama walikuwa wamekurupushwa kwenda kwenye mchezo ule wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho.

Kama Simba wangekuwa makini wangerejea kile kipigo cha 6-0, sema ni tatizo ya wachezaji za zama hizi kuridhika na matokeo mapema. Kwa timu za wenzetu wanapopata nafasi ya kucheza na timu pinzani dhaifu wanapiga nyingi. Jumapili iliyopita Yanga ilistahili kupigwa nyingi.

Kwani ilipoteana tangu mapema kwenye mchezo huo. Bila ya shaka viongozi na wadau wa klabu hiyo ya Jangwani wamejifunza kitu kupitia kipigo hicho.

Advertisement

Wanatakiwa kuamka sasa na kuanza kuijenga timu yao kwa msimu ujao. Kama watajiaminisha wamefungwa kwa hila na watani zao na kubweteka, watarajie kuburuzwa tena na Wekundu wa Msimbazi, kwa sababu wenzao wana timu bora na inayojituma uwanjani.

Tuachane na hayo, ili nisiwatie uchungu Wana Jangwani, ila kidogo leo naubadilisha upepo.

Nikumbushe tu, Jumamosi ya Aprili 7, 2012 huwa naikumbuka sana na naamini ni vigumu kwangu kuisahau pengine kwa sababu ya fani niliyonayo.

Naikumbuka kwa vile tangu alfajiri nilipoamka nilikuwa napata jumbe mfupi za maneno na wakati mwingine kupigiwa simu nikiulizwa juu ya kifo cha aliyekuwa nyota wa filamu za Kibongo nchini, Steven Kanumba.

Awali, ujumbe uliponifikia kwa mara ya kwanza katika simu yangu, nilihisi huenda ilikuwa utani ama aliyenitumia alichanganya na siku ya Karume Day iliyokuwa ikiadhimishwa siku hiyo, lakini ukweli ukabaki kuwa Kanumba alikuwa amefariki dunia kwenye ugomvi wake na aliyekuwa mpenziwe, Lulu.

Marehemu Kanumba akazikwa na watu wakaanza kumsahau, huu ni mwaka wa nane tangu staa huyo alipofariki dunia nyumbani kwake, Sinza na kuzikwa makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Kifo cha Kanumba kimeacha pengo kubwa, sio kwa familia yake ama ndugu na jamaa zake, lakini hata katika tasni ya uigizaji nchini. Hakuna siri alikuwa amepiga hatua kubwa na kuwaacha wenzake mbali.

Alijitotautisha na wengine katika sanaa yake hata kama alipitia Kaole Sanaa Group iliyowaibua magwiji wa filamu za Kibongo nchini.

Aliiona fursa na kuichanganyikia, kazi zake zilibamba ndani ya nchi na zilishafuka nje ya nchi akishirikiana na nyota mbalimbali wa Nollywood.

Kifo chake kilitokea akiwa ametoka kuiingiza sokoni filamu yake ya Devil’s Kingdom aliyoigiza na Nouah Ramsey mbali na filamu nyingine zilizojumuisha wakali wa Nigeria kama kina Mercy Johnson, Bimbo Akintola, Nancy Okeke, Nkiru Sylvanus na wengine.

Bahati mbaya ni kwamba aliowaacha nyuma ni kama wamelala usingizi wa pono na kuishia kulialia tu wakipinga kazi za nje zisiingizwe nchini.

Kisingizio ni kwamba hazilipiwi kodi na zinalibania soko la filamu za Kibongo.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba kabla ya Bongo Movie kuingia sokoni, filamu za kigeni zilikuwapo, tulikuwa tukiziangalia filamu za Kidosi, za kichina, Kinigeria, za kizungu na nyingine.

Pia hata enzi za Kanumba biashara hiyo ilifanyika na hakuna aliyekuwa akilalamika. Kwa wanaokumbuka filamu za Kibongo zilikuwa zikiuzwa bei kubwa kuanzia Sh 5,000-7,000 wakati zile za nje zikiwa chini ya bei hiyo, lakini watu walizipotezea kazi za nje na kukimbilia filamu za Kibongo.

Hii ni kwa sababu zilileta mapinduzi kwa watazamaji kupenda vya nyumbani na waliofanya fani hiyo kipindi hicho walichangamka na kuumiza vichwa kutengeneza kazi nzuri hata kama nyingine zilinakiliwa toka kazi za kigeni na kuigizwa kiswahili.

Kanumba na wenzake kipindi hicho, walijikita katika kutengeneza kazi zenye ubora na viwango vilivyoteka watazamaji walioamua kuzipa kisogo filamu za Kinigeria, Kihindi, Kichina na nyingine.

Leo kila muigizaji ama shabiki wa filamu za Kibongo ukiuliza sababu ya kushuka kwa soko la kazi za nyumbani, majibu yake ni kwamba kazi za nje ndio tatizo na wengine kudai Kanumba kaondoka na tasnia hiyo.

Sikubaliani na hoja hizo, ni kweli Kanumba alikuwa mjanja na aliweza kulisimamisha soko kwa kuangalia mbali kama ambavyo leo mwimbaji Diamond alivyofanya kwenye muziki na kuwaacha wenzake mbali.

Lakini, tatizo ni waigizaji na watayarishaji wa filamu waliosalia, wamekubali kufa kikondoo. Wamekubali kuliruhusu soko la kazi za kigeni kurejea tena kwa kasi kwa kuandaa kazi za ovyo, zisizo na uhalisia wala kuvutia mtazamaji.

Pia wanashindwa kwenda na kasi ya dunia ya sasa ya kuuza kazi mtandaoni lakini zikiwa kwenye ubora unaohimili soko la kimataifa.

Filamu karibu zote sokoni zinafanana maudhui na waigizaji ni wale wale, mavazi yale yale na mandhari ni yale yale na mbaya zaidi ni kwamba hadithi zinarudiwa na kurudiwa mpaka inaudhi. Waigizaji wanatumia muda mrefu kutengeneza skendo magazetini kuliko kujichimbia lokesheni kutengeneza kazi zenye kuuzika, kazi zitawezaje kupenda kwenye filamu za kizungu?

Advertisement