Kifo cha Manu Dibango pigo lingine tasnia ya muziki

Muktasari:

Dibango aliyekuwa mahiri kwa kupuliza 'midomo wa bata', yaani Saxaphone na Vibraphone anakumbukwa zaidi na nyimbo yake matata la Soul Makossa lilitoka mwaka 1972.

Dar es Salaam.Tasnia ya muziki duniani imezidi kupata pigo kipindi hiki cha ugonjwa wa corona, baada ya gwiji mwingine, Manu Dibango wa Cameroon kufariki kwa virusi vya ugonjwa corona.

Kifo cha mkali huyo wa Afro-Jazz, inaelezwa amekumbwa na mauti asubuhi ya leo Jumanne kwenye hospitali ya mjini Paris, Ufaransa baada ya kukumbwa na covid-19 akiwa na umri wa miaka 86.

Dibango jina lake kamili ni Emmanuel N'Djoke Dibango amefariki dunia wakati dunia ikiendelea kuomboleza vifo vya wanamuziki wengine Aurlus Mabele wa Congo Brazzaville na Kenny Rogers mkali wa Country waliofariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mabele alifariki dunia akiwa Ufaransa kwa kilichoelezwa ni saratani, huku Rogers alikumbwa na mauti akiwa nyumbani kwake nchini Marekani kwa kifo cha kawaida.

Dibango aliyekuwa mahiri kwa kupuliza 'midomo wa bata', yaani Saxaphone na Vibraphone anakumbukwa zaidi na nyimbo yake matata la Soul Makossa lilitoka mwaka 1972.

Katika wimbo huo kuna kibwagizo kilichowahi kumponza Michael Jackson kwa kukitumia katika nyimbo wake 'Don't Stop the Music' kabla ya Rihanna naye kukitumia akidhani ulikuwa na WackoJacko katika ngoma yake ya Wanna be Startin Somethin.

"Tunasikitika kutangaza kumpoteza Manu Dibango, kilichotokea leo Jumanne', taarifa katika ukurasa maalum wa mwanamuziki huo wa facebook ulisomekana na kueleza mazishi yake yatafanyika bila kuhuhusisha watu, ingawa haikutajwa ni wapi.

Mkali huyo aliyezaliwa, Desemba 12, 1933 katika mji wa Douala, alinza sanaa ya muziki miaka mwaka 1968 hadi alipokuwa na mauti akipiga miondoko asilia ya Cameroon 'Makossa', African Rhumba, Afro funk na Afrobeat jazz.

 Mbali na kuimba na kupuliza saxa, Dibango alikuwa pia ni mtunzi na alikuwa mmoja ya wanamuziki waliokuwa kama nembo ya Afrika kutokana na umahiri wake kwenye muziki, huku mashirika mbalimbali ya kimataifa ikiwamo UNICEF kuwa balozi.

Enzi za uhai wake amefyatua albamu kadhaa na kutamba ni nyimbo nyingi kali baadhi yake ni kama Soul Makossa, Big Blow, New Bell, The Panther, Sun Explosion, Aye Africa, Oh Koh, Pepe Soup, Super Kumba, O Bosso, Soir Au Village, Afrcan Boogie, Ekedy, Mangabolo, Senga, Bayam Sell'am, Soul Fiesta na Dikalo.

Marehemu ameacha watoto watatu Georgia, Marva na Michael Dibango.