Kanye West, mastaa kibao wapinga ubaguzi

Friday June 5 2020

 

Mwanamuziki, Kanye West ameongezeka katika listi ya mastaa mbalimbali duniani walioamua kuunga mkono kampeni ya kupinga unyanyasaji na ubaguzi uliotokea Marekani mwezi uliopita.
Kampeni hiyo ambayo imeambatana na maandamano katika nchi mbalimbali, ilianza mara baada ya Polisi wa Marekani kumuua kwa kumkanyaga shingoni raia wa nchi hiyo mwenye asili ya Afrika, George Floyd (46), tukio lililotokea Mei 25 huko Minnesota.
Marekani inakadiriwa kuwa na watu zaidi ya milioni 328 ambapo kati ya hao, watu weusi ni asilimia 13.4
West aliungana na waandamanaji wengine jana Alhamisi kutembea katika mitaa ya Chicago ikiwa ni ishara za kupinga unyanyasaji na ubaguzi wa watu weusi nchini humo na duniani kwa ujumla.
Mbali na kushiriki maandamano hayo, West pia ameanzisha Mfuko Maalum uitwao '528 College Saving Fund' kwa lengo la kukusanya kiasi cha Dola 2 milioni (zaidi ya Sh 4 bilioni) kwa ajili ya kuchangia Wamarekani wenye asili ya Afrika ambao katika siku za hivi karibuni wameuliwa na Polisi au watu weupe.
Mke wa Kanye West, Kim Kardashian alisema kuwa wameamua kuungana na wengine ili kutafuta usawa.
"Mimi na timu yangu tunasimama kuungana pamoja na wote wanaopaza sauti zao kupigana na mfumo kandamizi wa haki za binadamu," alisema Kardashian.
Kujiunga kwa mwanamuziki huyo na mkewe Kardashian ni muendelezo wa kundi kubwa la mastaa duniani ambao wameunga mkono kampeni na harakati hizo.
Mastaa wengine walioonyesha kuguswa na suala hilo la ubaguzi ni wanasoka Jadon Sancho, Thomas Muller, Marcus Thuram, klabu za Liverpool, Chelsea na Simba, Salma Hayek, mwanasoka wa Manchester United, Anthony Martial na mkewe Melanie, Achraf Hakimi na wengine.

Advertisement