Idris Sultan, mwenzake wajadiliana na DPP kumaliza kesi

Dar es Salaam. Upande wa utetezi katika kesi inayomkabili mchekeshaji Idris Sultan na mwenzake Innocent Maiga umedai kuwa washtakiwa hao wapo kwenye mazungumzo na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP), kwa ajili ya kuomba msamaha na kukiri makosa yanayowakabili.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kushindwa kufanya usajili wa laini ya simu ambayo ilikuwa inamilikiwa na mtu mwingine kinyume cha sheria.

Hatuna hiyo imekuja baada ya wakili wa Serikali, Kijja Luzingana kudai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Rashid Chaungu kuwa shauri hilo lilikuja katika mahakama hiyo kwa ajili ya kusikikilizwa ushahidi.

"Leo tuna shahidi mmoja na tupo tayari kuendelea na ushahidi,"alidai Luzingana ndipo wakili wa utetezi, Francis Mwakifuna alidai washtakiwa hao wapo kwenye mazungumzo  kwa ajili ya kuomba msamaha na kukiri makosa yanayowakabili.

"Wakili anayeendesha shauri hilo yupo katika Mahakama ya Rufaa na tumeleta hoja za kuomba msamaha na kukiri makosa yanayowakabili, hivyo tupo kwenye mchakato," alidai Mwakifuna.

Hakimu Chaungu aliutaka upande wa utetezi kabla ya Agosti 27, 2020 uwe umeshawasiliana na wakili wa Serikali na utakapofika mahakamani tarehe hiyo uwe na majibu.

"Upande wa mashtaka mnapokuja tarehe ijayo muwe na majibu mmefikia wapi kuhusiana na suala hilo," aliagiza Hakimu Chaungu.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 78/2020 ambapo katika shtaka la kwanza linalomkabili Sultani inadaiwa kuwa alishindwa kufanya usajili wa laini ya simu ambayo ilikuwa inamilikiwa na mtu mwingine, kinyume cha sheria.

Inadaiwa kuwa Sultan alitenda kosa hilo kati ya Desemba Mosi, 2019 na Mei 19, 2020 katika eneo la Mbezi Beach, ambapo alitumia laini ya simu iliyomilikiwa na Innocent Maiga bila kuripoti kwa mtoa leseni.

Katika shtaka la pili linalomkabili Maiga, mshtakiwa huyo anadaiwa kushindwa kutoa taarifa ya mabadiliko ya umiliki wa laini ya simu kwa kwa mtoa leseni.

Maiga anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Desemba Mosi 2019 na Mei 19, 2020 katika eneo la Mbezi Beach wilayani Kinondoni.

Inadaiwa katika siku hiyo ya tukio akiwa mmiliki halali wa laini hiyo alishindwa kutoa taarifa ya mabadiliko ya namba ya simu kama inatumiwa na Idris Sultan, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.