Hatimaye safari ya Ruge duniani imemalizika

Tuesday March 5 2019

 

By Rhobi Chacha na Phinias Bashaya

RUGE Mutahaba amemaliza safari yake duniani. Ilikuwa saa 10:04 jioni, jeneza kubwa lililokuwa na mwili wake, linateremshwa kaburini huku mamia ya waombolezaji wakiwa kimya wakati tukio likiendelea.

Hiyo ni baada ya kiongozi wa ibada kusema sasa mwili wa Ruge uwekwe kwenye nyumba ya milele. Hapo ndipo sura za waombolezaji zikabadilika. Kila mwenye kitambaa alikuwa akifuta machozi.

Kila mmoja alikuwa akivuta hisia zake na ndizo zilizosababisha kushindwa kuzuia machozi. Ilikuwa ni ishara kwamba Ruge hatutamwona tena. Safari yake ya duniani imetimia na sasa amelala kwenye nyumba yake ya milele.

Ruge alifariki Alhamisi iliyopita nchini Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa matatizo ya figo ambayo yalikuwa yakimsumbua tangu Oktoba mwaka jana.

Baada ya kumalizika kwa shughuli za kuaga jijini Dar es Salaam zilizoongozwa na Rais John Magufuli, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na viongozi wengine, wabunge, mawaziri, wasanii na wananchi mwili wake ulisafirishwa hadi Bukoba kwa maziko.

Kama ilivyokuwa Dar es Salaam, shughuli nzima ilikuwa katika Kijiji cha Kiziru, Kata ya Karabagaine, Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.

Advertisement

MAMA ATAKA WOTE WAMZIKE MWANAWE

Mama mzazi wa Ruge, Christina alitia ngumu mwili wa mwanawe kuondolewa katika Viwanja vya Gymkhana mpaka wananchi wote wanaotaka kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa mtoto wake watakapoisha.
Wasimamizi wa shughuli hiyo walitaka kukatiza utaratibu kutokana na wingi wa watu wanaotaka kumuaga Ruge. Hatua hiyo ililazimika kuendelea hadi sehemu kubwa ya waombolezaji wakatoa heshima zao.

Msafara wa magari uliondoka baada ya zoezi hilo kukamilika magari yakiwa yamejipanga yakiongozwa na gari maalumu lililobeba mwili.

Awali wakati wa tukio la kuaga mwili wake katika Viwanja hivyo vya Gymkhana, Maaskofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba walimtaja Ruge kama kijana jasiri mzalendo na mfano wa kuigwa.

Askofu Desderius Rwoma ameitaka jamii kuenzi mambo mema aliyoacha huku msaidizi wake.

Mwingine aliyetoa neno ni Askofu Methodius Kilaini alisema vijana wengi wamepata mafanikio kutokana na uthubutu wake na ujasiri wa kusimamia anayoamini.

NYUMBA YA MILELE

Ibada ya maziko iliongozwa na Katibu wa Parokia ya Itahwa, Anathory Kyatwa huku nyimbo za kabila la Wahaya zikipamba tukio la maziko.

Baada ya kuongoza taratibu za kuweka mwili kwenye kaburi huku nyimbo zenye ujumbe wa neno la Mungu ukiendelea na baadaye ukafuata utaratibu wa kuweka mashada ya maua.

Miongoni mwa walioweka mashada ya maua ni Wabunge mbalimbali akiwemo Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye na Wilfred Lwakatare pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.

WASANII WAMZIKA RUGE

Msanii wa muziki kutoka THT Dito alisoma salamu kutoka THT na kusema: “Ruge alikuwa mtu muhimu sana na hata ulipokuwa ukimkosea sana Ruge, alikuwa hakati tamaa na wewe wala kukuchukia.
“Alikuwa mtu wa kusamehe na kuanza maisha mapya na kutupa muda wa kusimamia kazi zetu na kujipanga upya.”
Aidha alisema kuwa Ruge alipenda kuwaambia kuwa waishi kwa usawa na kupendana, kupambana lakini pia heshima kwa watu wote.

Katika mazishi hayo, wasanii mbalimbali walioshiriki mwanzo mwisho kuonyesha namna gani marehemu Ruge aliwagusa wengi ni pamoja na Mrisho Mpoto, Harmonize, Bushoke, MwanaFA na Shilole.

Pia Nandy ambaye hata hivyo aliwekwa eneo la tofauti kwa kuwa ni mzazi mwenzake na Ruge.

Nandy alishiriki kuweka shada la maua sambamba na wanawake waliozaa na marehemu Ruge.

SALAMU ZA CCM

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya CCM, Heri James alisema taifa limepoteza kijana mzalendo ambaye fikra zake zimewavusha vijana wengi.

Advertisement