Harmonize awatoa wasanii nje ya boksi

Friday October 11 2019

 

By Rhobi Chacha

BAADA ya msanii wa Bongo Fleva Harmonize kutangaza ujio wa mgahawa wake alioupa jina la Konde Boy, amewataka wasanii kutotegemea zaidi muziki, bali wawekeze pia nje ya kazi hiyo.

Harmonize amesema wapo baadhi ya wasanii ambao wana uwezo kutokana na muziki lakini wanategemea muziki, ila maisha yao ni magumu.

“Hauwezi kutegemea muziki peke yake ukasema utakuwa na maisha mazuri, msanii anayejitambua lazima atafute biashara nyingine hata kama muziki unalipa, lakini hauwezi kufikia yale malengo ambayo umeyapanga. Ni wachache sana wenye bahati hiyo,” anasema Harmonize.

“Hivyo msanii anatakiwa kujiongeza, wengi tunawaona walivyoishia katika maisha mabaya kutokana na wao kuwekeza kwenye muziki pekee bila kujua maisha ya baadae yatakuwaje.”

Harmonize anayetamba na wimbo ‘Inabana’ ameliambia Mwanaspoti kuwa ameamua kujitoa kwa jamii baada ya kusema anafungua mgahawa utakaokuwa unatembea mtaa kwa mtaa ili kuwalisha watu wasiojiweza.

Alieleza kuwa hilo ni kutokana na taarifa aliyoichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram wiki chache zilizopita alipoandika ‘Kidogo na kingi Mungu ndie hutoa na yeye ndie kamuumba masikini na tajiri...!!!! Hata hapa nilipo ni kwa neema zake sitokula na kusaza ikiwa kuna wengine kula yao ni ya shida, nitagawana nao.”

Advertisement

Huu utakuwa uwekezaji wa kwanza nje ya muziki ambao Harmonize atakuwa ameufanya tangu Tanzania imfahamu na ni wasanii wachache waliofanikiwa kufanya uwekezaji nje ya muziki wao wanaoufanya.

Harmonize ambaye aliomba kuondoka lebo ya WCB ambayo aliingia nayo mkataba wa zaidi ya miaka 10, hivi karibuni ameteuliwa kuwania tuzo ya Mwanamuziki Bora wa Afrika 2019 katika tuzo za MTV Ulaya ambako anakabiliwa na ushindani kutoka kwa wanamuziki wa Afrika Kusini - Nasty C na Prince Kabyee, Toofan na Burnaboy.

Uteuzi huo unamfanya Harmonize kuwa ndiye msanii wa tatu wa muziki wa Afrika Mashariki kuwahi kuteuliwa kutoka Afrika Mashariki na Kati.

Iwapo atashinda tuzo hiyo atajiunga na mwajiri wake wa zamani kutoka WCB, Diamond Platnumz na AliKiba ambao waliwahi kushinda tuzo hiyo kwa miaka miwili mfululizo wakifuatana.

Mshindi wa tuzo ya muziki wa Afrika anapata fursa ya kuendelea katika ngazi ya kimataifa na kushiriki katika kitengo cha muziki wa Asia dhidi ya muziki wa Afrika.

Shindano hilo linatarajia kutafanyika Novemba 3, 2019 mjini Seville, Uhispania huku mchakato wa kupiga kura ukiwa wazi sasa.

Advertisement