Duma: Mahaba kidogo tu mnaomba tuachane?

Sunday October 25 2020
duma pic

KAMA ulikuwa hutarajii kuona ‘couple’ mpya Instagram mwaka huu baada ya ile ya Shilole na mpiga picha wake Rammy kuibuka hivi karibuni, nakushauri shusha chini matarajio yako kwani ndio kwanza Oktoba, kwa hiyo kuna zaidi ya siku 60 zimebaki za 2020.

Na kwa kukuthibitisha hilo, tayari kuna couple mpya kwenye mitandao ya kijamii ambayo inatusumbua kwa kutupia picha mpya karibu kila baada ya dakika 60. Ukiikosa kwenye Insta story, basi wapo kwenye Instagram Feed au Snapchat au kwenye status zao za Whatsapp — Couple ya muigizaji Duma na bi dada ambaye pia ni mcheza filamu kutoka Kenya, Mishi Dora.

Hata hivyo, licha ya kwamba Duma yupo kwenye gemu kwa zaidi ya miaka mitano sasa na akiwa ameshashiriki kazi kubwa ikiwemo tamthilia ya Siri ya Mtungi na filamu zake kama vile Nipe Changu aliyozindua kwenye ukumbi wa Sinema Mlimani mwaka 2018, hakuwahi hata siku moja kutuonyesha mpenzi wake Instagram. Kiasi kwamba alipoanza kutupia picha hizi za sasa, watu wakahisi jamaa kahakiwa nini?

Sasa Vibe ya Mwanaspoti ilimtafuta Duma na kumtaka afunguke ukweli wa kile tusichokijua kuhusu mapicha picha ambayo ya mekuwa yakishambuliwa kwa ‘comment’ nyingi mbaya kama vile; ‘Mwanamke mbaya’ na ‘Mwanamke mkubwa kuliko mwanaume.’

NI PENZI TU

Kwanza Duma alikiri kwamba akaunti yake haijawahakiwa, zile picha zote za mabusu na mahaba zinazopostiwa ndiye anayeziachia na kinachomsukuma kufanya hivyo ni mapenzi.

Advertisement

“Sijawahi kuposti mpenzi wangu Instagram, lakini kwanini sasa hivi? Kwa sababu nimeona ndio muda sahihi, na kinachonisukuma kufanya hivi ni mapenzi,” anasema Duma.

Akiwajibu wanaosema anafanya kiki kwa sababu labda anajiandaa kuachia filamu mpya, Duma anasema hajawahi kufika kufanya kazi kwa kutumia kiki. “Niko kwenye gemu muda mrefu, tangu naigiza kazi za watu mpaka sasa hivi nafanya kazi zangu mwenyewe, hata siku moja sijawahi kutumia kiki, kwanini sasa hivi? Siamini katika kiki ila najua kinachowachanganya watu ni kwamba hawajanizoea kuniona hivi,” anasema Duma ambaye jina lake kamili ni Daudi Michael.

KUHUSU PISI YENYEWE

Akimueleza mwanamke wake Duma anasema ni muigizaji kutoka Kenya ambaye wapo kwenye uhusiano kwa takribani miaka mitatu sasa. Na pia amekuja Tanzania kwa ajili ya mipango yao ya ndoa inayotarajiwa kufungwa hivi karibuni hapa Bongo kisha baadaye ndoa nyingine ya kimila itafungwa Kenya.

“Nimefahamiana na mke wangu mtarajiwa tangu mwaka 2017, na amekuja kwa ajili ya mipango ya harusi yetu. Nilishaenda kwao, nilishakamilisha kila kitu, tunasubiri harusi tu, na tutawaambia ni lini muda ukifika.” anasema. Anasimulia kwamba yeye na mwanamke wake huyo walikutana Mombasa nchini Kenya wakati Duma alipokwenda kuigiza filamu moja nchini humo.

“Mimi na yeye tulikuwa tunaigiza kama mke na mume kwenye filamu hiyo. Tukaona kama ‘chemistry’ zetu zinaendana hivi, kwa hiyo tukaamua kwanini isiwe kweli. Na sasa tuko hapa.”

 

Advertisement