Dada wa Godzilla asimulia rapa huyo alivyohangaika kabla ya kufikwa na umauti

Dada wa marehemu aelezea kifo cha Gozilla

Muktasari:

  • Mkali wa Hip Hop nchini Tanzania Godzillah amefariki dunia leo asubuhi Jumatano Februari 13, 2019 huku dada yake Joyce Mbunda akieleza jinsi mwanamuziki huyo alivyohangaika saa chache kabla ya kifo chake.

Dar es Salaam. Joyce Mbunda, dada wa mwanamuziki wa Hip Hop, Godzillah aliyefariki dunia leo Jumatano Februari 13, 2019  amesema ndugu yake aliteswa na kitu kilichokwama tumboni kwa zaidi ya siku tatu na kumfanya atapike mfululizo.

Akizungumza leo nyumbani kwao Salasala jijini Dar es Salaam, Joyce amesema mwanamuziki huyo Golden Mbunda alikuwa akitapika kwa siku tatu mfululizo.

Amesema rapa huyo aliyewahi kutamba na wimbo  Lakuchumpa alianza kujisikia vibaya na alipokwenda hospitali alibainika kuwa na malaria, sukari kuwa juu na presha.

“Jumapili (Februari 10, 2019) alilala muda mrefu, haikuwa kawaida. Baadaye akaomba barafu tulivyompa akaanza kutapika ndipo tulipompeleka hospitali na kugundulika ana malaria, sukari imepanda sana na presha imeshuka,” amesema.

“Pia marehemu alisema kuna kitu kiling’ang’ania tumboni kama vile kinataka kutoka ila kinagoma, alijaribu kukitoa kwa kujitapisha lakini hakikutoka.”

Pamoja na kupata nafuu baada ya matibabu alilalamika kitu hicho kuendelea kukwama tumboni.

“Alipewa ruhusa ingawa alikuwa anaendelea kutapika. Usiku akaanza kuishiwa nguvu. Tukamrudisha hospitali akawekewa dripu mwisho akaandikiwa dozi ya siku 10. Alipofika nyumbani alisali kabla ya kuingia kulala lakini haikuchukua dakika 10 akaanza kuniita,” amesema.

“Nilimfuata chumbani nikiwa na mama, akatuambia naona watu wengi wananifuata wamezunguka nyumba wanataka kunichukua. Akainuka ghafla akasema acha nitoke nje, tukamshika maana alikuwa anaihangaika akamlalia mama na hakuinuka tena.”

Amesema walimpeleka hospitali ya jeshi ya Lugalo wakiamini kuwa anaweza kuwa amezimia tu lakini waliambiwa amefariki dunia.