Alikiba akataa mwaliko wa Diamond kwa kurusha kijembe

Muktasari:

Mapema leo Diamond alitoa taarifa ya kutaka kuonana na uongozi wa Alikiba kwa lengo la kumwalika kushiriki katika tamasha la Wasafi litakalofanyika Novemba 9 mwaka huu.

Dar es Salaam. Mwanamuziki Alikiba amekataa mwaliko aliopewa na Diamond wa kushiriki tamasha la Wasafi Festival akiandika katika ukurusa wake wa Instagram asiletewe mambo ya darasa la pili.

Mapema leo Diamond alitoa taarifa ya kutaka kuonana na uongozi wa Alikiba kwa lengo la kumwalika kushiriki katika tamasha la Wasafi litakalofanyika Novemba 9 mwaka huu.

Kiba amejibu hayo kupitia ukurasa wake wa Instagram akiandika 'Usiniletee mambo ya darasa la pili unaniibia penseli alafu unanisaidia kutafuta (Unikome)'.

"Mwanaume huwa anaongea mara moja tu sasa ukitaka nikuweke uchi watu wajue unavyonifanyia hata kwenye hilo tamasha hatakuja mtu sasa tuishie hapo nakutakia tamasha njema Diamond," ameandika Alikiba.

Tukio la kuhusishwa kwa Alikiba kualikwa kwenye tamasha hilo haliajaanza mwaka huu ni baada ya Novemba 2018 kutokea taarifa kama hizo ambapo Diamond aliahidi kukutana na uongozi wa nyota huyo ili aweze kushiriki.

Mwaka jana AliKiba alisema ameshukuru kwa kupata mualiko wao ila hataweza kushiriki kutokana na kuwa na majukumu mengine ya kuzindua kinywaji chake cha Mofaya Energy.

Mbali na hilo Kiba alimuomba Diamond kudhamini tamasha hilo ili kusongesha gurudumu la muziki wa Tanzania.

"Pia ndugu zangu Wasafi tumepata "Salamu zenu (Wasafi) nimepata. Nashukuru kwa mualiko wenu, ila kwa bahati mbaya sitoweza kushiriki kwa sasa kutokana na majukumu ya kuzindua Mofaya katika nchi zingine. Hata hivyo tusingependa kuwaacha hivi hivi, tupo tayari kuwapa support ya kudhamini tamasha lenu kupitia MofayaEnergyDrink ili kuweza kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya sanaa yetu Tanzania na Africa.