Akaunti za wasanii zatajwa kusafirisha dawa za kulevya

Muktasari:

Rais Shirikisho la Filamu ameeleza namna akaunti feki za wasanii maarufu zinavyotumika kwenye biashara ya dawa za kulevya.

 Rais wa Shirikisho la Filamu, Simon Mwakifamba ametoboa siri jinsi wasanii wanavyotumika katika kusafirisha dawa za kulevya.

Mwakifamba ameyasema hayo leo Jumatano kwenye kongamano kuhusu tatizo la dawa za kulevya kwa wasanii lililoandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo linafanyika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere.

Mwakifamba amesema wakati awali walitumiwa wachezaji na wanamasumbwi lakini sasa hivi wanatumiwa wasanii wa fani nyingine ikiwemo muziki na filamu.

Amefafanua kwamba kwa wasanii wa muziki wafanyabiashara hao wamekuwa wakitumia akaunti feki kujitambulisha kuwa wao ni wasanii jambo ambalo ni uwongo. "Baadhi ya nchi, ukishatambulisha wewe ni msanii wanakuchukulia kwa uzito wa hali ya juu, na wanaogopa kukufanyia baya lolote wakijua huenda ukaichafua nchi yao. "

 

Hivyo hasa wafanyabiashara hushirikiana na baadhi ya watu kufungua akaunti feki za wasanii maarufu, na wanapofika huko huwaonesha mamlaka za usalama pale wanapohojiwa maswali na baada ya kufanikiwa kupita viwanja vya ndege, akaunti hiyo hufutwa,"ameeleza Mwakifamba.

Hata hivyo aliishukuru Tume ya Dawa za Kulevya kutambua umuhimu wa wasanii na Kuwaita katika kampeni hiyo ya kupambana ma dawa za kulevya.

Alitumia nafasi hiyo kuwaomba wasanii wenzake kwenda kuwa mabalozi wazuri wa vita hiyo na kueleza kuwa ukweli ni kwamba msanii akifanya jambo zuri ni rahisi jamii kuiga na akifanya baya na rahisi pia kuigwa.