ALIKIBA AMEIKOMESHA ILE DHARAU YA KIMUZIKI

Muktasari:

Ukomavu wa kipekee ni kiwango cha Alikiba cha kucheza kimepaa, uzuri zaidi anaimba na kucheza. Alikiba wa sasa ni mwanamuziki aliyekamilika.

HESABU mwaka 2013 kurudi nyuma, Alikiba alikuwa anatajwa kuwa mwanamuziki asiye na makali jukwaani. Vile shoo zake zilikuwa za playback, na madansa wake hawakuwa na kipya, ndivyo dharau ilikuwa nyingi.

Mwaka 2012, rapa Roma Mkatoliki alinitamkia waziwazi kuwa Alikiba hakuwa na ukali wowote jukwaani kumlinganisha na Diamond.

Ni ile 50 Mentality, kwamba hakuna kupokea dharau, bali ikija inatakiwa ipewe pigo takatifu ili salamu zirudi kwa waanzisha dharau kisha washike adabu zao.

Kufikia mwaka 2014, Alikiba alikuwa ameshafanya mabadiliko makubwa ya shoo zake jukwaani. Alivutia alivyoimba na alivyocheza pamoja na madansa wake. Alinoga sana na mdogo wake, Abdul Kiba.

Agosti 2015, wakati wa hafla ya wasanii kumuaga Rais wa Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, Alikiba alipofanya shoo ya live band, hakuwa mzuri. Alifunikwa sana na watoto wa Yamoto Band; Aslay, Mboso, Beka na Enock Bella.

Alikiba alipwaya sana. Sauti yake ilionesha ni kijana mwanafunzi wa kupiga live. Pamoja na hivyo, ukweli haukubadilika kuwa ubora wake ulikuwa unaongezeka.

Kutoka Agosti 2015 mpaka mwaka 2017 ni takriban miaka miwili. Hapo katikati sikupata bahati ya kushuhudia shoo yoyote ya Alikiba jukwaani. Mwaka 2017 nilimuona Alikiba wa daraja la juu sana. Uwezo wake wa kuimba jukwaani uliimarika na sauti ni yenye ukomavu.

Kiwango cha Alikiba cha kucheza kimepaa, uzuri zaidi anaimba na kucheza. Kwa heshima kabisa anaimba live. Alikiba wa sasa ni mwanamuziki aliyekamilika.

Wakati wengine wamekuwa mabingwa wa kelele jukwaani, mtu hajaimba hata nusu wimbo, anaiambia hadhira ipige kelele, mara wanyooshe mikono juu. Alikiba ameshapita mbali huko. Akifika jukwaani anajua nini ambacho watu wanataka ili waende naye pamoja. Alikiba ni mtoa huduma bora kabisa.

Leo hii ukiniuliza ni mwanamuziki gani ananivutia sana kumshuhudia akifanya kazi yake jukwaani? Jawabu halitachelewa, ni Alikiba. Amekomesha ile dharau iliyokuwa ikimwandama, eti hajiwezi jukwaani.

Hiyo ndio ambayo mwanamuziki 50 Cent huita 50 Mentality. Kwa nini watu waseme huwezi wakati una uwezo wa kufanya mageuzi na kila mmoja akakuogopa? Alikiba amefanya na anatisha sana.

Watu ambao walikuwa wanaonekana ni mahiri jukwaani kuliko Alikiba enzi hizo, kwa sasa wanayo mengi ya kujifunza. Sauti bora, yenye ukomavu, uwezo wa kucheza na kuimba, kwa umuhimu kabisa ni pumzi. Alikiba wa sasa anaweza kupiga shoo live kwa zaidi ya saa mbili na haboi.

Kuna mambo ya kubishana kuhusu wanamuziki, vipawa vya kutunga na kuimba na wingi wa mashabiki, lakini sio la kupiga shoo kali live. Alikiba amevuka viwango vingi, wakati huohuo wanamuziki wengi wanashuka. Pengine kwa kubweteka au kutojifunza zaidi.

Haya mambo ya kupanda jukwaani na kuimba playback hayana ishu tena. Ndio maana watu umri ukienda kidogo wanaona shoo za Bongo Fleva sio daraja lao, kwani wakihudhuria hakuna jipya zaidi ya kupigishwa kelele na kuambiwa waweke mikono juu.

Alikiba kwa sasa anaweza kuandaa shoo executive na naweza kulipa kiingilio hata cha Sh100,000, maana anastahili. Ni kwa sababu nina uhakika nikifika nitaona ufanisi halisi wa mwanamuziki jukwaani. Nikiondoka kurudi nyumbani sitafyonza.

Wanamuziki wengine wana kila sababu ya kujifunza kutoka kwa Alikiba kuhusu namna ya kuishinda dharau. Wafanye mazoezi na bendi, waziweke vizuri sauti zao. Waache kupafomu shoo za kisela.

Inasikitisha sana kuona mwanamuziki ambaye ameshapata umaarufu mkubwa, lakini akiwa jukwaani, hatofautiani na maandagraundi. Kipi spesho cha kuwashinda wengine? Kusema piga kelele inamshinda nani? Na kuamrisha watu wainue mikono juu kuna anayeshindwa?

Halafu kinachofuata na kuacha wimbo unacheza, msanii haimbi, badala yake anarukaruka jukwaani, kisha anamwambia DJ asimamishe muziki ili aongee na hadhira. Stori nyingi zisizo na mbele wala nyuma. Muda wa kuongea unakuwa mrefu kuliko wa kuimba.

50 Mentality ni kuchukia dharau na kupambana kuishinda. Kama Alikiba alivyoishinda dharau ya kuonekana mchovu jukwaani na leo kawa moto wa kuotea mbali mpaka inatakiwa wengine wajifunze kwake, ndivyo kila mmoja anaweza.

Alikiba angeridhika na ile dharau naye leo angekuwa walewale. Naye angekuwa mpiga kelele na kurukaruka jukwaani badala ya kuimba. Kwa sasa, ukiacha mafundi wa muziki wa dansi, Alikiba ndio mwanamuziki mkali zaidi wa kumtazama jukwaani Afrika Mashariki. Hizo ngazi amepanda kwa sababu amekomesha dharau.

Na kwa vile dharau ameshaikomesha, hana budi kuongeza heshima. Namtazama mbali sana kama ataamua kuendeleza moto wake wa kupiga shoo za kiwango cha juu. Playback awaachie wazembe. Yeye apige muziki wenye hadhi yake.