Wema kumkuta ya Sitti Mtemvu

Tuesday September 29 2020
wemaaaa pic

HUENDA mrembo Wema Sepetu akakutwa na kashfa kama iliyomkuta Miss Tanzania mwaka 2014, Sitti Mtemvu ya kudanganya umri.

Hili limebainika baada ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), kueleza kusikitishwa na taarifa zake alizozitoa jana Jumatatu  kuhusu ukweli wa umri wake.

 Jana  Jumatatu, Septemba 28, 2020, Wema  ambaye alikuwa Miss Tanzania mwaka 2006 aliibua gumzo baada ya kutamka ana miaka 30 umri ambao ni tofauti na aliokuwa akiusema awali.

 Gumzo hilo lilizidi kupamba moto mitandaoni hasa watu walipopiga hesabu za miaka aliyoshiriki shindano la Miss Tanzania na kugundua kuwa alishiriki akiwa na miaka 16 jambo ambalo ni kinyume na sheria za shindano hilo ambalo linamtaka mshiriki awe ana miaka kuanzia 18 hadi 23.

 Kutokana na sakata hilo ambapo mpaka leo bado limeendelea kuteka vichwa vya habari na kuzungumziwa mitandaoni, Mwanaspoti Online imezungumza na BASATA kama msimamizi mkuu na mtoaji wa kibali cha mashindano hayo.

 Katika maelezo yake, Katibu Mtendaji wa baraza hilo,  Godfrey Mngereza, amesema watahakikisha wanafuatilia suala hilo kwa kuwa hawako tayari kuona sanaa inanajisiwa kwa watu kutoa taarifa za uongo na ukizingatia hayo mashindano ya Urembo nayo yana vigezo vyake na heshima zake katika sanaa ya nchi hii.

Advertisement

Mngereza amesema hata mwaka 20014 ilipotokea kwa Sitti Mtemvu waliamua kuingilia kati na hatua stahiki zilichukuliwa na mwisho wa siku akavuliwa taji lake na kupewa mwingine.

 “Kwa Sitti mliona tulivyofanya, hivyo hata kwa Wema hili halitushindi pamoja na kuwa alishinda taji hilo zamani, lakini haituzuii kuchukua hatua ambapo tutashirikisha na mamalaka nyingine,” amesema.

 Alipoulizwa kama kuna malalamiko wamewahi kupata enzi za Wema alipotawazwa kuwa Miss Tanzania, Mngereza amesema hana uhakika na kuahidi kurejea katika nyaraka zao kwa kuwa wakati huo hakuwa Katibu katika Baraza hilo.

 Hata hivyo wakati Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA),  wakisema kisheria hawawezi kumchukulia hatua Wema mpaka pale itakapotokea mtu amepeleka malalamiko Polisi na wao kubaki kama mashahidi.

 Basata wamesema taarifa hizo za mitandao  zinaweza kuwa moja ya chanzo  pia kwao ambapo watamuita Wema kuthibitisha kama ni yeye aliandika kabla ya hatua zaidi.

 “Wema katika kufuatilia hili lazima tumuhusishe maana haya mambo ya mitandao huwezi jua labda akaunti yake watu waliiba kwa muda na kuyaandika hayo hatuwezi tu kujidhihirisha kwa upande mmoja,” amesema Mngereza.

 Endapo sakata la umri la Wema kama lingeshikiwa bango mwaka ule alioshiriki Miss, basi Jokate Mwegelo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe kwa sasa ndio angekuwa Miss Tanzania baada ya kushika nafasi ya pili katika mashindano hayo huku nafasi ya tatu ilienda kwa Lisa Jensen na namba nne alikuwa ni Irene Uwoya.

Advertisement