VIDEO: Diamond achangia upasuaji wa moyo kwa watoto 10 JKCI

Muktasari:

Kampuni ya Wasafi WCB imechangia Sh80 milioni matibabu ya moyo kwa watoto 40 kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ikiwa ni fedha zilizotokana na michango ya wasanii walio katika kampuni hiyo, nje ya kampuni, wadau na Watanzania wa ndani na nje ya nchi.

Dar es Salaam. Mwanamuziki Diamond amechangia Sh20 milioni kwa ajili ya upasuaji wa moyo kwa watoto 10 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Diamond jina lake halisi ni Naseeb Abdul ni Mkurugenzi wa WCB amechangia kiasi hicho cha fedha huku wanamuziki wengine walio ndani na nje ya kampuni WCB na wadau wakichangia Sh60 milioni.

Fedha hizo zimepatikana baada ya kampuni ya WCB kuchangisha kiasi cha Sh80 milioni kupitia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Watoto hao wanatimiza idadi ya watoto 90 watakaofanyiwa upasuaji kufikia Desemba na kuvuka idadi ya ahadi aliyoiweka Makonda ya watoto 60 waliotoka katika familia duni kupatiwa matibabu hayo kuanzia Juni 24 mpaka Desemba mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kutembelea wodi za watoto na vyumba vya upasuaji leo Jumanne Novemba 5, 2019 Diamond amesema yeye aliweka idadi ya watoto 10 kuwafikia na tayari ameshalipa kiasi cha Sh10 milioni kama kianzio kwa watoto watano na wiki ijayo atatoa kwa wengine watano.

“Nimepita katika wodi mbalimbali kwa kweli nimeumia watoto wanaumwa na wazazi wao wana hali duni ni ngumu kumudu gharama hizi za matibabu, kupitia kipindi cha Block 49 Wasafi FM tumeweza kuzungumza na Mkuu wa mkoa Makonda na akaeleza hali halisi mimi nilichanga, wasanii wangu pia wakachanga, kupita kipindi tukapata michango mingi kutoka kwa wasanii wa ndani na Watanzania wengine waliopo nje,” alisema Diamond.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda amesema tangu atoe ahadi yake, leo ni mara ya tano anafika JKCI na tayari ameshatimiza kwa watoto 40 na wengine 10 watafanyiwa upasuaji mapema wiki hii na ijayo.

“Niliahidi watoto 60 kufikia Desemba, mpaka sasa watoto 40 wamefanyiwa upasuaji kwa msaada wa mashirika mbalimbali na wengine 10 watafanyiwa wiki hii. Ilikuwa nimebakiza watoto 10, lakini nikamwambia Diamond nina watoto pale JKCI na wewe ninakulea, akasema nitachangia watoto 10. Tulifanya kampeni kupitia kipindi cha redio na tukapata mchango utakaotosha kuchangia watoto 30 hivyo nimevuka lengo,” alisema Makonda.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohammed Janabi amesema Taasisi hiyo ina watoto 512 wanaohitaji upasuaji kwa sasa wengi wao wapo majumbani.

“Wanaumwa na wanahitaji msaada wa haraka, hatuwezi kuwaweka hapa wote hatuna nafasi. Kwa sasa tunao 27 ambao wanaendelea kupokea huduma za upasuaji, tatizo ni kubwa kwani kwa kila watoto 100 mmoja anazaliwa na tatizo la moyo na kwa takwimu za mwaka 2018 walizaliwa watoto milioni 2 hivyo kufanya jumla ya watoto 13,000 kuhitaji huduma za upasuaji,” alisema Profesa Janabi.