#WC2018: Wazee wa kumwaga maji

KWENYE soka kuna msemo unaopamba kwa sasa. Ukisikia mwagaa, ujue hapo inamaanisha kuwa ipigwe krosi ndani ya boksi, watu wajitwishe.

Mara nyingi shughuli hiyo imekuwa ikifanywa na mabeki wa pembeni kwa mfano tu, kule Chelsea kuna mtu huyo anaitwa Cesar Azpilicueta kiboko kwa kumwagia Alvaro Morata, ambaye amekuwa akijitwisha kwelikweli kwa wababe hao wa Stamford Bridge.

Bahati mbaya tu pacha hiyo haitakuwapo kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia, kwa sababu Morata hakujumuishwa kwenye kikosi cha Hispania.

Lakini, joto la fainali hizo za Russia likizidi kupanda, mashabiki watakwenda kushuhudia wakali wa kupiga krosi ndani ya boksi, ambao kwenye soka la kisasa, wanaitwa wakali wa kumwaga maji!

Hawa hapa, wakali watano wa kumwaga maji utakaokwenda kuwashuhudia kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Russia kuanzia mwezi ujao ambapo mataifa 32 yatashuka uwanjani kuwania ubingwa huo wa dunia.

Marcelo, Brazil

Kuna asiyemfahamu Marcelo kweli? Fundi wa mpira huyu anayecheza kwenye kikosi cha Real Madrid na huko kwenye fainali za Kombe la Dunia atakuwa kwenye uzi wa Brazil. Marcelo ni beki wa kushoto, lakini staili yake ya kucheza kila wakati unamwona kwenye eneo la wapinzani na uhodari wake wa kupiga krosi umemfanya amtengenezee mabao mengi sana Cristiano Ronaldo wanapocheza pamoja huko Bernabeu.

Lakini, kwenye fainali za Kombe la Dunia kitu atakachokwenda kufanya ni kuhakikisha Gabriel Jesus anapata krosi zake kwa wingi ili kuifungia mabao ya kutosha Brazil kwenye harakati zao za kufukuzia ubingwa.

Neymar na washambuliaji wengine wa Brazil akiwamo Jesus watakwenda kuzichoka krosi zake Marcelo kwenye fainali hizo za Russia.

Danny Carvajal, Hispania

Pale Real Madrid, kushoto akiwa Marcelo, basi kulia kuna mtu anaitwa Danny Carvajal.

Wote wanaifahamu vizuri kazi ya kumwaga maji. Uzuri wa Carvajal ukiweka kazi ya kupiga krosi kali, anafahamu vyema pia shughuli yake ya kukaba kupita maelezo. Kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika huko Russia, mashabiki watamshuhudia Carvajal akiwa ndani ya jezi za Hispania, wababe wengine hawa wanaokwenda kupigania ubingwa.

Kasi yake ya pembeni upande wa kulia kwenye kupandisha mashambulizi imempa uwezo wa kuwahi kupiga mipira ya krosi kwa washambuliaji wa kati kitu ambacho kwenye fainali za huko Russia ni wazi, beki huyo wa kulia atakwenda kumfanya Diego Costa awe bize kupasia nyavuni kwa kichwa.

Benjamin Mendy, Ufaransa

Mwanzoni mwa msimu wa Ligi Kuu England uliomalizika wiki za karibuni kwa timu yake ya Manchester City kubeba ubingwa, Benjamin Mendy alikuwa akimwaga maji balaa. Alikamatia namba kwenye beki ya kushoto ya Man City kumpiga benchi Danilo hadi hapo alipokuja kupata majeruhi ambayo yalimzindua Fabian Delph na kuanza kupata nafasi ya kucheza katika kikosi hicho cha Pep Guardiola.

Hata hivyo, alirejea siku za mwisho mwisho za kufunga msimu na Kocha Didier Deschamps amemjumuisha kwenye kikosi chake cha Ufaransa kitakachokwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia.

Mendy atakwenda kuwafanya Antoine Griezmann na Olivier Girous kuwa bize kwa zile krosi zake matata ambazo amekuwa akipiga na hilo ndilo linalowafanya Ufaransa kuwa moja ya timu tishio kwenye fainali hizo za Russia.

Danny Rose, England

Manchester United imeripotiwa kuhaha kupata huduma yake. Danny Rose bonge la beki la kushoto kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur na shughuli yake si ya kitoto.

Naye atakuwapo Russia akiwa na kikosi cha England, ambacho kwenye shavu la kulia kutakuwa na mtu mwingine anayeitwa Kyle Walker, ambaye pia kiboko pia kwa kupiga mitungi ya maana kwenye boksi.

Lakini, Gareth Southgate atakwenda kupata raha kutoka kwa mabeki wake hao wa pembeni, hasa Danny Rose, ambaye hakika atakwenda kumfanya Harry Kane kuonyesha ule umahiri wake wa kupiga vichwa kutokana na krosi za wakali hao kutoka pande zote kushoto na kulia. England ina utajiri wa wakali wa kupiga krosi, kwani kwenye kikosi chake kuna mtu mwingine anaitwa Kieran Trippier.

Joshua Kimmich, Ujerumani

Kama kuna kitu kigumu unachopaswa kufanya, basi ni kumzuia Joshua Kimmich asimwage maji anapokuja kwenye eneo la karibu la goli lako. Beki huyo wa pembeni wa Bayern Munich ni fundi wa kupiga krosi hatari. Kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Russia atakuwamo kwenye kikosi cha mabingwa watetezi, Ujerumani.

Kama vile nawaona Thomas Muller na wenzake watakavyokuwa bize kujitwisha krosi zake atakazokuwa akizimimina kwenye goli la timu pinzani. Ujerumani inaamini ina kikosi kilichosheheni mastaa wenye uwezo na mmoja wa wakali wake ni Kimmich akiwa na uhodari mkubwa wa kupiga krosi zitakazoleta mabao kwa timu yake.

Pakua HAPA jarida letu la #KombelaDunia2018 la WIKI HII linaloletwa kwako na magazeti uyapendayo ya MWANANCHI na MWANASPOTI.