Wanaweza kumrithi Pluijm Singida

HABARI za uhakika ni kwamba msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, Singida United itamkosa kocha wake Mkuu, Hans van Pluijm ambaye anatajwa kutimkia Azam FC kwa ajili ya kuanza maisha mapya.

Hans ambaye ameiongoza Singida United kwa msimu mmoja akitokea Yanga, ameisaidia kuwa ndani ya tano bora kwenye msimamo wa Ligi Kuu, huku akiifikisha katika Fainali ya Kombe la FA.

Tangu kutua kwa Mholanzi huyo nchini mwaka 2013, amekuwa na mafanikio makubwa katika kazi yake ya soka. Mafanikio makubwa aliyapata Yanga ambako alishinda mataji manne tofauti.

Kutokana na soka safi pamoja na mafanikio ya Singida msimu huu, ni wazi Singida United inahitaji kupata kocha mwenye uwezo wa juu wa kurithi mikoba yake.

Ikumbukwe Singida inatarajia kucheza Fainali ya Kombe la FA Juni 2, dhidi ya Mtibwa Sugar na kuna dalili zote za timu hiyo ya mkoani Singida kupata tiketi ya kuiwakilisha nchi katika Mashindano ya Kimataifa mwakani.

Kutokana na hali hiyo, lazima uongozi wa timu hiyo uumize kichwa kutafuta kocha mwenye uwezo ambaye ataweza kuhimili mikiki mikiki ya michuano hiyo mikubwa.

Mwanaspoti inakusogezea orodha ya makocha kadhaa ambao wanaweza kuwa mbadala wa Hans kwenye kikosi cha Walima Alizeti hao.

Ettiene Ndayiragije

Kocha huyu raia wa Burundi anaweza kuisaidia Singida United katika mechi zake za mashindano tofauti kutokana na uwezo wake katika kuandaa vijana kiushindani.

Pia elimu yake katika soka inambeba kwani ana Leseni A inayotambulika na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) na kipindi ametua hapa nchini kuinoa Mbao, kazi yake ilionekana.

Ndayiragije licha ya baadaye kukutana na vizingiti kutoka kwa mashabiki wa Mbao baada ya timu kutopata matokeo mazuri, lakini msimu uliopita hata klabu za Simba na Yanga zilivutiwa naye.

Hata hivyo inadaiwa Mrundi huyo tayari ameshafanya mazungumzo na vigogo wa Singida United kuweza kuinoa msimu ujao.

Mafanikio yake ya kuifikisha Mbao FC katika fainali ya Kombe la FA mwaka jana, ndiyo inambeba zaidi, pamoja na kandanda safi ililokuwa ikitandaza Mbao.

Masoud Djuma

Singida United labda wakose pesa za kumlipa tu, lakini tofauti na hapo Kocha Djuma kama atatua klabuni hapo, anaweza kuwasahaulisha kabisa habari za Pluijm.

Mfumo wake na kutengeneza morali kwa vijana umempa mafanikio makubwa kocha huyu msaidizi wa Simba na hadi sasa anachekelea na ubingwa wa Ligi Kuu.

Tulishuhudia Simba ikihaha kwa zaidi ya misimu mitano mfululizo bila kutwaa ubingwa, huku ikiajiri na kufukuza makocha mbalimbali, lakini ujio wa kocha huyo kutoka Burundi umekuwa wa neema kwa Wekundu hao wa Msimbazi.

Djuma alitua nchini kuchukua mikoba ya Jackson Mayanja kama kocha msaidizi akisaidiana na Mcameroon Joseph Omog, kisha kukaimu nafasi ya kocha mkuu kabla ya ujio wa Mfanransa, Pierre Lechentre.

Omog alifungiwa virago baada ya Simba kuondoshwa hatua za awali za Kombe la FA na timu ya Daraja la Pili, Green Warriors na kumwachia kazi Djuma ambaye kwa kiasi kikubwa amefanya kazi nzuri.

Abdalah Mohamed ‘Bares’

Kocha huyu anayekinoa kikosi cha Prisons anaweza kuwa suluhisho na mbadala wa Hans pale Singida United kutokana na uwezo aliouonyesha kwenye msimu huu wa Ligi Kuu.

Bares ameisaidia timu yake kuwa nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu, pia amekifanya kikosi hicho kuwa tishio kwa klabu kubwa za hapa nchini zikiwamo Simba, Yanga na Azam.

Falsafa na mbinu zake za kukijenga kikosi katika hali ya ushindani imemfanya kocha huyu Mzanzibar kuwa kocha mwenye mafanikio na timu hiyo.

Ammas Niyongabo

Kocha huyu anayekinoa kikosi cha Stand United naye yumo japo havumi, kwani ilishuhudiwa mwanzoni mwa msimu wa Ligi Kuu timu hiyo ikipata matokeo yasiyoridhisha, lakini chini ya mbinu zake, kwa sasa Stand inapumua.

Mrundi huyu kwanza aliisaidia timu hiyo kufika hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la FA, jambo ambalo liliwashinda makocha waliotangulia akiwamo Patrick Liewig na Hemed Morroco.

Kwa kutumia uwezo wake huku akisaidiana na msaidizi wake, Athuman Bilal ‘Bilo’, ameweza kutengeneza kikosi ambacho kimekuwa na ushindani tofauti na misimu iliyopita.

Bakari Shime

Kocha Bakari Shime ‘Mchawi Mweusi’ hakuna asiyemjua katika kufundisha soka la kujiamini na kiushindani na amedhihirisha hilo mara kwa mara.

Alianza na Mgambo JKT. Akaibeba mabegani mwake. Mgambo iliendelea kusalia Ligi Kuu kutokana na kudra za Shime na alipoondoka ikashuka.

Akaja kwenye timu ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys. Akaipeleka kwenye mashindano ya Afrika kule Gabon. Huyu ndiye Shime maarufu kama Mchawi Mweusi. Akathibitisha pia na JKT Ruvu. Aliikuta iko hoi, akashuka nayo daraja na kuipandisha. Siyo mtu wa mchezo mchezo.

Akiwa na kikosi chake alichopandisha Ligi Kuu, kocha huyu alihakikisha anaziadabisha timu alizokutana nazo kwenye mashindano ya Kombe la FA mwaka huu kabla ya kukwama kwa Singida United kwenye mchezo wa nusu fainali.

Kwa mantiki hiyo, Singida kama inahitaji mafanikio, basi kwa kocha huyu itakuwa imepatia sana katika kufikia malengo yake hapo mbeleni.

Wengine ni Mecky Mexime anayekinoa kikosi cha Kagera Sugar na Ally Bizimungu (Mwadui FC).