Ukiwa na majembe haya, Hazard wa kazi gani

Muktasari:

  • Kwa mchango wa Hazard aliotoa kwenye kikosi cha Chelsea chenye maskani yake huko Stamford Bridge, ni mchezaji ambaye hakika haitakuwa kazi rahisi kupata mbadala wake wakati atakapoamua kuondoka kikosini humo.

SUPASTAA Eden Hazard, kwenda Real Madrid ni uvumi ulioibuka upya tena kwa kasi na ripoti zinadai fowadi huyo wa Kibelgiji ametengewa Pauni 200 milioni kuhakikisha anatua Los Blancos mwishoni mwa msimu.

Kwa mchango wa Hazard aliotoa kwenye kikosi cha Chelsea chenye maskani yake huko Stamford Bridge, ni mchezaji ambaye hakika haitakuwa kazi rahisi kupata mbadala wake wakati atakapoamua kuondoka kikosini humo.

Hata hivyo, wanasema hakuna kiatu kisichomfaa mwingine, kama Hazard ataachana na maisha ya Stamford Bridge na kwenda Santiago Bernabeu, basi kuna mastaa kibao ambao kama watanaswa, basi The Blues watakuwa wanapiga tu miluzi na hawatakuwa na presha ya kuikosa huduma ya Mbelgiji huyo.

Achana na washambuliaji sijui kina Andy Carroll na Peter Crouch wanaodaiwa kuwindwa na Chelsea kwenye dirisha hili, wachezaji ambao watakuja kuwafanya wababe hao wa Stamford Bridge wamsahau kabisa Hazard atakapokwenda Real Madrid ni hawa hapa.

Mesut Ozil

(Arsenal)

Pengine ni jina ambalo hata mashabiki wa Chelsea wenyewe watakuwa wanalifikiria. Kiungo mchezeshaji wa Arsenal, Mesut Ozil, yupo kwenye miezi ya mwishoni ya mkataba wake Arsenal, hivyo kama msimu utamalizika na hajasaini dili jipya, basi atakuwa huru kwenda kujiunga na timu yoyote atakayopenda.

Kutokana na hilo, Chelsea itakachopaswa kukifanya ni kuharakisha kuinasa huduma ya Mjerumani huyo kwa sababu hatapatikana kirahisi kutokana na kuwindwa na timu nyingine pia ikiwamo Manchester United.

Chelsea kwa sababu itampoteza Hazard kwenda Real Madrid, hakuna ubishi Ozil ni mmoja kati ya wachezaji ambaye atakuja kuwasahaulisha The Blues machungu ya kuondokewa na supastaa wao wa maana.

Marco Asensio

(Real Madrid)

Taarifa zinadai straika Alvaro Morata anautaka sana uhamisho huu utokee, yaani wa Marco Asensio kwenda Chelsea wakacheza pamoja kwenye safu ya ushambuliaji ya miamba hiyo ya Stamford Bridge.

Kwa sababu Asensio ni mchezaji wa Real Madrid, basi Chelsea wanaweza kutumia ujanja wa kumtaka mchezaji huyo pamoja na pesa juu ili kumruhusu Hazard kwenda kwenye timu yao kama watahitaji huduma yake.

Siku za karibuni, Real Madrid imeripotiwa kuwa na mpango wa kufanya usajili wa wachezaji wa maana mara tu dirisha la mwisho wa msimu litakapofunguliwa na kwenye orodha ya wachezaji inaowataka, Hazard anahusika. Hazard alijiunga na Chelsea akitokea Lille ya Ufaransa mwaka 2012.

Antoine Griezmann

(Atletico Madrid)

Jina kubwa lililohusishwa na karibu klabu zote kubwa za Ulaya. Antoine Griezmann amekuwa kwenye ubora mkubwa huko Atletico Madrid na ndio maana jina lake limekuwa halikauki kutajwa kwenye korido za klabu kubwa za Ulaya. Alianza kuhusishwa na Manchester United, Real Madrid na Barcelona kabla ya sasa kutajwa kwamba huenda akanaswa na Chelsea kwa sababu wanaona wazi watampoteza Hazard kwenda Santiago Bernabeu.

Kulikuwa na ripoti pia kwamba Griezmann anatakiwa na Manchester City ambao wanataka kufanya dili la kubadilishana na Sergio Aguero. Lakini, kwa sasa Chelsea hawana namna zaidi ya kutazama uwezekano wa kumnasa Mfaransa huyo ili awapunguzie machungu ya wakati huo Hazard atakapoondoka.

Gareth Bale

(Real Madrid)

Ni kama itakavyotokea kwa Asensio, kuwasili kwa Hazard kwenye kikosi cha Real Madrid hakuna ubishi kutamfanya Gareth Bale kuwa na ruhusa ya kuondoka kwenye timu hiyo, la sivyo atakumbana na matatizo makubwa.

Staa huyo wa kimataifa wa Wales maisha yake ndani ya Bernabeu yamekuwa ya kupanda na kushuka, hivyo kama Los Blancos watamsajili Hazard, basi hali itakuwa mbaya zaidi kwa upande wake. Chelsea wanapaswa kuliona hilo na kuchangamkia fursa haraka.

Thomas Lemar

(Monaco)

Hivi karibuni alihusishwa na Chelsea. Wababe hao wa Stamford Bridge wanacheki uwezekano wa kumpata winga huyo wa AS Monaco ikiwa ni maandalizi tu ya awali kama watampoteza supastaa wake, Hazard kwenda Real Madrid.

Lemar kwa sasa amekuwa gumzo Ulaya nzima kutokana na kusakwa na timu vigogo baada ya kuonyesha kiwango kikubwa msimu uliopita kwenye Ligue 1 na Ligi ya Mabingwa Ulaya.