NINACHOKIAMINI: Ni Tanzania au Simba na Yanga za kuchagua uwanja?

Tuesday September 12 2017

 

By Frank Sanga

SUALA la mabadiliko si jepesi, huwa ni mchakato mgumu kwa sababu huhusisha mambo mengi mageni.

Binadamu kwa kawaida huingia woga, hupenda kufanya mambo kwa mazoea na huwa hawapendi kufanya majaribio ya mambo mapya.

Mbaya zaidi ni watu ambao wamejenga kasumba kuwa, baadhi ya vitu haviwezekani.

Badala yake yanapofanyika mabadiliko yoyote huwa wanabaki kushangaa.

Kuna watu walikuwa hawaamini kuwa Simba au Yanga zinaweza kucheza katika Uwanja wa Chamazi unaomilikiwa na Azam FC.

Walijaribu kutoa sababu mbalimbali, ambazo sikuona kama zina mashiko lakini zilijaa siasa kuhalalisha hoja zao.

Kuna ambao walidai uwanja huo unaobeba mashabiki 7,000 ni mdogo kwa hiyo Yanga au Simba ziwe zinailazimisha Azam kucheza Uwanja wa Uhuru au Taifa kwa sababu zina mashabiki wengi.

Wengine walisema uwanja huo upo mbali na pia hali ya usalama haiwezi kuwa nzuri kwa sababu mashabiki wengi watajitokeza na itakuwa ngumu kuwadhibiti.

Azam na Simba zimecheza mwishoni mwa wiki katika mchezo wa suluhu kwenye uwanja huo, lakini hakuna jambo baya limetokea.

Visingizio vyote sasa vimeshindwa na hiyo ina maana kuwa mechi zote ambazo Azam ni mwenyeji zitachezwa kwenye Uwanja wa Chamazi.

Tunapaswa kujua kitu kimoja ambacho ni umuhimu wa uwanja wa nyumbani.

Ndio maana kuna mechi za nyumbani na mechi za ugenini.

Uwanja wa nyumbani siku zote huwa mzuri kwa timu mwenyeji na kamwe hauwezi kuwa mzuri kwa timu ngeni.

Simba haiwezi kunufaika na uwanja wa Chamazi tofauti na wenyeji Azam.

Azam hawana mashabiki wengi, kwa hiyo wananufaika kucheza kwenye uwanja wao kwa sababu Simba haitapata nafasi ya kuwa na mashabiki wengi.

Simba wanakosa nguvu ya kuwa na mashabiki wengi kwa sababu wako ugenini.

Tukumbuke kuwa Uwanja wa Manchester United, una uwezo wa kujaza watu 75,000 pale Old Trafford, lakini huwezi kusikia timu hiyo ikilalamikia inapokwenda St Mary’s kucheza na Southampton FC.

Uwanja wa Old Trafford unachukua watu 75,000, lakini uwanja wa St Mary’s unabeba mashabiki 32,000 kwa hiyo lazima tujue tofauti ya viwanja vya nyumbani na ugenini. Machester United wakiwa nyumbani wanapata faida ya mashabiki, wakiwa ugenini hawapati nafasi hiyo.

Tena kwa nchi hizo za Ulaya, suala si uwanja tu, lakini timu mwenyeji huamua hata idadi ya tiketi za kuipa timu ngeni.

Nadhani hilo tunaweza kulichukua hata hapa kwetu, kwamba timu mwenyeji awe anachukua tiketi asilimia kubwa kuliko timu ngeni.

Ninachoshukuru ni kuwa ilimradi mechi ya Azam na Simba imefanyika vizuri sioni kama mjadala huu unapaswa kuendelea, badala yake ni vyema sasa tukasonga mbele na tuwaache Azam wafurahie matunda ya uwanja wao.

Ni ukweli usiopingika kuwa Simba na Yanga zina mashabiki wengi nchini, lakini mpira una kanuni zake na mmoja ya kanuni hizo ni kuwa kutakuwa na uwanjani wa nyumbani na ugenini.

Mbali na hilo, hiyo ya kuchezea Azam Complex kwa Simba na Yanga ni changamoto.

Kucheza kwenye uwanja wa Azam, labda wajitoe ufahamu, lakini kama wana ufahamu wao, wanatakiwa kujipanga kuwa na wao kuwa na viwanja vyao.

Kama leo wamecheza mbele ya mashabiki 7,000 wa Azam, wajipange wajenge viwanja vyenye mashabiki zaidi ya hao ili kuionyesha Azam kuwa na wao wanaweza kuwa na chao lakini pia ni wakongwe, zaidi ya hapo, kila mara wataendelea na aibu kutokuwa na uwanja.