MAYANGA VS MKWASA: Rekodi zenyewe zinaongea

MAYANGA

Muktasari:

  • Bahati mbaya wanaopiga kelele dhidi ya Mayanga wanasahau kuwa namba hazidanganyi.

NAMBA hazidanganyi bwana! Kama utaona namba zinadanganya, basi ujue kuna mawili, ama hesabu zimekosewa au hila imefanyika. Ila daima namba huwa hazidanganyi kabisa.

Tangu Kocha Salum Mayanga alipokabidhiwa Taifa Stars Januari 2, mwaka huu imepita miezi 11 sasa. Kuna baadhi ya mashabiki wamekuwa wakiiponda timu yake. Wanaliponda soka lake na namna timu inavyobadilika badilika kila mara uwanjani kama kinyonga.

Wapo wanaomponda kwa namna anavyobadilisha wachezaji kila mara na hata mfumo wake wa kujiamini hauendani na soka la Stars ya Kocha, Boniface Mkwasa aliyemwachia mkoba huo.

Mkwasa alipewa Stars Juni 23, 2015 akipomkea Mart Noij na kukaa nayo kwa muda wa miezi kama 18 kabla ya Shirikisho la Soka Tanzaia (TFF) kusitishia mkataba wake kutokana na kiwango kisichoridhisha. Kelele zimezidi baada ya juzi kati Stars kupata matokeo ya sare nchini Benin katika pambano la kirafiki la kimataifa.

Bahati mbaya wanaopiga kelele dhidi ya Mayanga wanasahau kuwa namba hazidanganyi. Ni kweli Stars ya Mayanga haina soka tamu na la kusisimua kama ambalo Stars ya Mkwasa ililicheza mbele ya Nigeria na Algeria jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Mayanga amemwacha mbali Mkwasa kwa rekodi, licha ya kuwa na kipindi kifupi.

Mwanaspoti linakuletea tofauti iliyopo baina ya makocha hao katika mechi walizoziongoza Stars.

IDADI YA MECHI

Mkwasa hana tofauti kubwa ya mechi aliyoiongoza Stars dhidi ya Mayanga. Licha ya kudumu na Stars kwa miezi 18, Mkwasa aliiongoza timu hiyo katika mechi 13, moja pungufu ya 14 alizoongoza Mayanga katika muda wa miezi 11 tu tangu kukabidhiwa kikosi hicho.

Kitu cha kushangaza ni kwamba, katika mechi hizo 13 za Mkwasa, tisa zilikuwa za mashindano kama Mayanga, huku nne zikiwa za kirafiki.

MATOKEO TOFAUTI

Kama kuna jambo ambalo Mayanga amemuacha mbali Mkwasa katika kipindi chao ndani ya Taifa Stars ni aina ya matokeo aliyokuwa akipata uwanjani. Mayanga katika mechi zake 14 ndani ya Stars, ameshinda michezo sita, huku saba akitoka sare na kupoteza pambano moja tu.

Hii ni tofauti na Mkwasa ambaye katika mechi zake 13 alifanikiwa kushinda mbili tu, huku akipoteza mara saba na minne ndio aliyotoka sare. Kwa mantiki hiyo ni kwamba Mayanga katika mechi zake 14 amekusanya pointi 25 dhidi ya 10 pekee alizoambulia Mkwasa ndani ya timu hiyo ya taifa.

MABAO NAKO MMH!

Ingawa Mayanga amekuwa akipondwa kwa kikosi chake kutocheza soka tamu na la kusisimua zaidi ya kujiamini, lakini ndiye aliyefanikiwa kuvuna mabao mengi kuliko Mkwasa.

Katika mechi aliyoiongoza Stars, Mayanga amewawezesha vijana wake kufunga mabao 16 dhidi ya manane ya Mkwasa, ikiwa na maana kila mechi ana wastani wa bao moja.

Katika eneo la kulinda lango, Mayanga yupo vizuri zaidi kwani katika mechi hizo 14 ukuta wake umetikiswa mara 10 tu, wakati kikosi cha Mkwasa kilifungwa mabao 22 ikiwa na wastani wa kuruhusu kama mabao mawili kwa kila mchezo waliocheza.

BADO KAZI IPO

Kwa sasa Mkwasa ni kama mtu anayepumua baada ya kuachana na kazi ya kuinoa Stars, lakini kazi kubwa anayo Mayanga hasa kuelekea kwenye mechi za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Afrika (Afcon) kule Cameroon, 2019.

Mayanga ameiongoza Stars katika mechi moja tu ya kundi lake la L dhidi ya Lesotho na kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani. Machi mwakani Stars itaifuata Uganda kabla ya kurudi nyumbani kuwapokea Cape Verde baadaye Septemba. Mkwasa alichemsha katika mbio za kufuzu fainali za CHAN 2016 akiipokea timu toka kwa Mholanzi, Mart Nooij aliyeiponza mapema Stars kwa kupigwa mabao 3-0 na Uganda.

Aliishia kulazimisha sare ya 1-1 Kampala na kushuhudia Stars iking’olewa, kabla ya kuchemsha kwenye mbio za kuwania fainali za Afcon 2017 na zile za Kombe la Dunia 2018. Mayanga amekwama kwenda kwenye fainali za Chan 2018 baada ya kutolewa na Rwanda na kazi anayo kwenye mbio za Afcon 2019.

TOFAUTI NDOGO

Kuna tofauti ndogo sana ya uchezaji wa Stars ya iliyokuwa ya Mkwasa na Stars ya sasa ya Mayanga. Stars ya Mkwasa ilikuwa ikitandaza soka safi na kushambulia kuanzia nyuma, huku ikitegemea zaidi viungo waliokuwa wakitengeneza mashambulizi makali. Kwa Mayanga licha ya kuwatumia viungo, lakini bado muda mwingi wamekuwa wakijihami.

Hata ukiangalia wastani wa kufunga mabao katika mechi zao, hakuna timu iliyoshinda au kufunga katika mechi moja zaidi ya mabao mawili, kuonyesha kuwa kuna utofauti ukubwa wa uchezaji wa timu za makocha hao mawili. Hivyo hata zile kelele kwamba, Mayanga hafai na ni mbovu kuliko Mkwasa ni mambo ya kishabiki tu, ila ukweli ni kwamba Stars za wawili hao hazijatofautiana sana na kinachombeba Mayanga ni matokeo mazuri aliyonayo mpaka sasa.

Amepoteza mchezo mmoja tu na ameruhusu mabao machache kulinganisha na Mkwasa aliyeongoza mechi moja pungufu na Kocha Mayanga.

Hivyo wanaomsakama Mayanga wanaweza kurudi kuzisoma upya namba kwa kuwa hazidanganyi, ila kama kuna ulazima wa mabadiliko basi tuachane na Mayanga, lakini tukimpa heshima yake katika kipindi kifupi alichokuwa na Stars basi itapendeza.