Kujitoa Kagame, Yanga haina hoja-2

Muktasari:

  • Sababu ambazo mabingwa hao mara tano wamezitoa hazina mashiko hata kidogo, kwa kifupi ni za kitoto mno kwani wiki iliyopita tuliona jinsi timu hiyo ilivyozoea kulumbana na wasimamizi wa soka tangu ilipoasisiwa Ligi ya Tanzania 1965. Endelea...!

MABINGWA wa kihistoria wa Tanzania, Yanga SC, wamegonga tena vichwa vya habari ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) baada ya kuandika barua kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakiomba kujitoa katika michuano ya Kagame Cup 2018.

Sababu ambazo mabingwa hao mara tano wamezitoa hazina mashiko hata kidogo, kwa kifupi ni za kitoto mno kwani wiki iliyopita tuliona jinsi timu hiyo ilivyozoea kulumbana na wasimamizi wa soka tangu ilipoasisiwa Ligi ya Tanzania 1965. Endelea...!

MWAKA 1966

Msimu uliofuata wa 1966, Yanga walizua malumbano mengine ili kupata sababu ya kususa ligi baada ya ‘kuchungulia’ na kuona ubingwa haupo huku ligi ikiwa katika mzunguko wa 13 ikibaki mitano na Yanga wakiwa nafasi ya tatu, Sunderland wakiongoza.

Watani wa jadi, Sunderland na Yanga walikutana kwenye mchezo wa pili wa ligi, Novemba 5, 1966.

Yanga walikuwa wanaongoza 2-0 hadi dakika ya 75 pale mchezaji wao mmoja alipolimwa umeme. Lakini hata hivyo, viongozi wake walimkataza kutoka, baada ya malumbano refa akavunja pambano.

FAT wakaamua mchezo urudiwe, mchezaji aliyesababisha mgogoro afungiwe michezo mitatu na nahodha wa Yanga afungiwe miezi 12. FAT pia ikaipa adhabu Yanga kukosa sehemu ya mapato yake ya mchezo ule.

Kwa kuwa Yanga walikuwa wanatafuta sababu ya kususa, basi wakawa wameshapata hivyo wakajitoa kwenye ligi.

Viongozi wa FAT na wa michezo mingine wakagundua kwamba Yanga walikuwa wanatafuta sababu...wakafuta adhabu zote ili Yanga wasijitoe.

Mwisho wa msimu, Simba waliibuka mabingwa na Yanga wakamaliza nafasi ya 4.

MWAKA 1967

Mwaka 1967, Yanga waligoma kushiriki wakisema hawana wachezaji kwa vile wachezaji wao wengi walisafiri na timu ya taifa iliyoenda Kinshasa (Zaire) kwa Kombe la Mataifa ya Afrika na wakitoka huko waunge moja kwa moja Nairobi Kenya kwa Kombe la Gossage (siku hizi Kombe la Cecafa Challenge).

Matukio ya Yanga kujikuta kwenye malumbano yasiyo na tija no mengi na kama ‘vichwa’ vinavyofanya maamuzi kwa niaba ya Yanga havitabadilika, basi tutarajie malumbano milele.

Kwa mfano mwaka 2003, Yanga waligoma kushiriki ya Ligi ya Muungano, mbaya zaidi, wakaenda kufungua kesi mahakamani!

Nani kasahau walipokataa kucheza mechi ya mshindi wa tatu Kombe la Kagame 2008? Kwa wanaokumbuka viongozi wa Yanga walitoa utetezi wa kitoto sana kwamba eti walikubaliana na wenzao wa Simba kugomea mchezo huo mpaka watakapohakikishwa mgao wa asilimia 50 kwa 50 kwa sababu wao ndio wanayoyabeba mashindano hayo yalipofanyika nchini. Vipi kuhusu Kombe la Kagame 2014 kule Rwanda walipotaka kupeleka ‘vitoto’?

Yanga (na hata pacha wake Simba) ni kitu kikubwa sana kwenye soka ndani ya nyoyo za watanzania, lakini yenyewe kiuhalisia ni ndogo sana...inaongozwa na vichwa vyepesi mno, ambavyo badala ya kufikiria namna ya kuisongesha mbele klabu, wao wanafikiria namna ya kususa na kuanzisha malumbano.

Hata ukifuatilia kwa undani sababu walizotoa kuyakacha mashindano yajayo ya Kombe la Kagame utabaini ni kasumba ile ile waliyokuwa nayo kwa miaka nenda rudi. Sijui ni lini watabadilika.