Kitakachoibeba Liverpool kutwaa ubingwa ulaya

Muktasari:

  • Wakati mwingine historia huwa zinajirudia. Inaweza kujirudia tena kwa Liverpool na kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka huu.

UNAWEZA kuikubali hii lakini pia unaruhusiwa kuikataa. Hulazimishwi kuikubali moja kwa moja kama huamini katika historia.

Wakati mwingine historia huwa zinajirudia. Inaweza kujirudia tena kwa Liverpool na kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka huu.

Historia hiyo hiyo, imeonekana kujirudia kwa Yanga ya jijini Dar es Salaam. Mabingwa hao wa Tanzania wenye maskani yao makutano ya Mitaa ya Twiga na Jangwani, wametinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, katika staili ileile ya mwaka 1998.

Mwaka huo, Yanga chini ya Kocha Tito Mwaluvanda iliitoa timu ya Ethiopia na kutinga hatua ya makundi Klabu Bingwa Afrika. Mwaka huu, imeitoa timu ya Ethiopia tena na kutinga hatua ya makundi Kombe la Shirikisho. Mwaka 1998 iliitoa Coffee FC na mwaka huu imeitoa Welaytta Dicha. Sikia na hii, Yanga kabla ya kuitoa Coffee FC. Wababe hao wa Ethiopia walitoka kuitoa Al Alhy ya Misri. Mwaka huu, timu nyingine ya Ethiopia iliyotolewa na Yanga, Welaytta nayo iliitoa timu nyingine ya Ethiopia kwenye hatua iliyopita. Welaytta iliitoa Zamalek.

Kama mambo yanaweza kutokea hivyo kwa kujirudia, kwanini ishindikane kwa Liverpool?

Ipo hivi. Mwaka 2005, wakati Liverpool inakwenda kufanya maajabu yake kule Uturuki kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kupigwa Tatu Bila hadi mapumziko kisha ikachomoa zote kwenye kipindi cha pili na kutwaa ubingwa kwa mikwaju ya penalti, matukio yake yaliyotokea msimu huo, yanafanana kabisa ya msimu huu. Katika msimu ule ambao Liverpool ilibeba ubingwa, ilimuuza mchezaji wake aliyekuwa akivaa jezi namba 10 kwenda kwenye timu ya Hispania. Alikuwa Michael Owen, aliyeuzwa kwenda Real Madrid. Mwaka huu, ikiwa tayari imeshatinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ya Ulaya, Liverpool imemuuza tena mchezaji wake aliyekuwa akivaa jezi namba 10 kwenda kwenye klabu nyingine ya Hispania. Ni Philippe Coutinho aliyetoka Anfield kwenda Barcelona. Sababu iliyomuondoa Owen huko Liverpool ndiyo ileile iliyomuondoa Coutinho, kutaka kwenda kubeba mataji. Mwaka 2005, wakati Liverpool inakwenda kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, msimu huo ilifungwa na mahasimu wao, Manchester United mabao 2-1 kwenye Ligi Kuu England.

Mabao ya Man United kwa kipindi hicho ambacho kilikuwa cha msimu wa 2004/05, yalifungwa na mchezaji mmoja, Mikael Silvestre, aliyefunga yote mawili, wakati lile la kujifariji la Liverpool lilikuwa la kujifunga, ambapo beki, John O’Shea alitupia kwenye wavu wake. Msimu huu imejirudia. Liverpool imepigwa tena 2-1, huku mabao ya Man United yakifungwa na mchezaji mmoja na lile la Liverpool likiwa la kujifunga pia. Marcus Rashford alifunga mabao mawili na lile la kujifunga, liliwekwa wavuni na beki Eric Bailly. Mechi hizo zote zilipigwa kwenye Uwanja wa Old Trafford. Chukua na hii. Msimu huo huo, ambao Liverpool ilibeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, iliitupa nje timu ya England kwenye muchuano hiyo, kama ilivyofanya msimu huu. Kipindi kile iliisukuma nje Chelsea na safari hii imeitoa Manchester City. Nakwambia historia inaweza kujirudia, kama unaamini lakini. Kipindi kile, mwaka huo 2005 wakati inabeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Liverpool kwenye kikosi chake kulikuwa na mchezaji wa kutoka Senegal, Salif Diao na mwaka huu ikielekea kufanya hivyo, kikosi chake kina Msenegali mwingine, Sadio Mane.

Msimu huu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, historia ya mwaka 1981 imejirudia tena.

Timu zilizotinga nusu fainali nchi zake hazina tofauti na zilizotinga nusu fainali ya mwaka huo ambapo Liverpool ilitwaa taji hilo. Kitu kinachovutia zaidi kwenye timu hizo, tatu ni zilezile za mwaka 1981, isipokuwa moja tu. Kipindi kile timu zilizotinga nusu fainali ni Inter Milan (Italia), Bayern Munich (Ujerumani), Real Madrid (Hispania) na Liverpool (England). Safari hii, zilizotinga nusu fainali ni AS Roma (Italia), Bayern, Liverpool na Real Madrid. Historia imeandikwa hapo kinchi na kitimu pia. Kipindi kile, Liverpool ndiyo ilibeba ubingwa. Bado tu huamini kama Liverpool itabeba ubingwa wa Ulaya msimu huu? Kwenye nusu fainali, wababe hao wa Anfield watacheza na AS Roma.