Huyu jamaa ndiye kila kitu kwa Msuva

JUZI Jumanne katika mfululizo wa makala za nyota wa kimataifa wa Tanzania anayecheza Morocco, Saimon Msuva tuliona jinsi makocha wa Difaa El Jadida na timu nyingine walivyochanganywa na umahiri wa staa huyo.

Msuva alipoondoka Tanzania akitokea Yanga, alikuwa akifahamika kama winga, lakini Morocco anacheza kama mshambuliaji namba mbili wa kati na anatupia sana nyavuni.

Mwenyewe anakiri haoni tatizo la kupangwa hapo kwani anafurahia. Lakini leo katika mwendelezo wa makala hizo, tutamwona mtu muhimu na aliye kaka baba wa Msuva ughaibuni.

Unamjua mtu huyo? Endelea naye...!

Mtu huyo bwana anaitwa Ali El Ataoui. Ndiye mtu muhimu zaidi katika maisha ya Msuva pale Jadida. El Ataoui, mtu mrefu kuliko wote katika benchi la ufundi la Jadida, ndiye baba na rafiki mkubwa wa Msuva katika maisha ya Morocco.

El Ataoui ni Kocha wa Saikolojia. Katika soka la Morocco kila timu ina mtu kama huyu katika benchi la ufundi. Huyu ndiye ambaye anawaangalia wachezaji kiakili kabla na baada ya mechi. Ndiye anayewahamsisha wachezaji na kusikiliza matatizo yao.

Bahati iliyopo kwa Msuva ni kwamba El Ataoui ndiye mtu pekee ambaye anaongea Kiingereza vizuri katika timu ya Jadida kwa jumla. Wengine wote wanaongea Kifaransa na Kiarabu. El Ataoui ndiye ambaye huwa anasimama karibu na Msuva pindi Kocha Taleb Abderrahim anapotoa maelekezo kwa timu yake. Humtafsiria kile ambacho kocha anaongea.

El Ataoui ndiye ambaye alimpokea Msuva Jadida na ndiye ambaye anazunguka naye kila mtaa, wanakula pamoja, wakati mwingine Msuva anakwenda kulala na familia yake. Hata wakati ninakwenda Morocco, El Ataoui ndiye aliyetumwa na Msuva kuja Uwanja wa Ndege wa Mohamed V jijini Casablanca kunipokea.

“Saimon ni kama mwanangu. Nimempokea hapa tangu siku ya kwanza na ninahakikisha maisha yake yote yanakwenda vizuri hapa. Unajua hawezi kuongea Kifaransa wala Kiarabu, hivyo ni jukumu langu kuwa karibu. Si unaona kama hivi? Nimekuja kukupokea kwa sababu alinipa taarifa zako zote majuzi,” anasema El Ataoui.

“Ni jukumu langu kuwa karibu na kila mchezaji, lakini nipo karibu zaidi na Msuva kwa sababu ni kijana mpole na mtaratibu, pia hapa kuna makundi mawili, kuna wachezaji wenzake wa kigeni ambao wanatoka nchi zinazozungumza Kifaransa, halafu kuna wachezaji wa Morocco ambao wanazungumza Kifaransa na Kimorocco. Sasa kama wale wa kigeni huwa wanatembea zaidi wenyewe ingawa bado ni marafiki wa Saimon,” anasema El Ataoui.

“Simon alipofika hapa niliona kipaji chake, lakini nikahisi kama vile anaweza kurudi Tanzania. Alikuwa mpweke hivyo kazi yangu ikawa kumtembeza dukani, sokoni, tunakula pamoja, nampeleka katika familia yangu ambayo wamemzoea sana. Hii ilikuwa mbinu ya kuinua morali yake,” anaongeza El Ataoui.

“Huwezi kuamini, kuna wakati nilikuwa ninakuja kulala hata kwa Saimon kwa ajili ya kuhakikisha anaondoa upweke. Mimi pia ndiye ambaye nilikuwa ninahahakisha mtu wa usafi anakuja kwa wakati na kumfanyia kazi zote za ndani. Unajua mchezaji ambaye ni mpweke hawezi kucheza soka vizuri. Ni tatizo kubwa,” anasema El Ataoui ambaye pia ni Mwalimu katika Chuo kimoja cha Jadida.

“Kama hakuna mechi mwishoni mwa wiki basi huwa tunaendesha na Msuva hadi kwa Mohamed kwa ajili ya kupumzika kule. Mke wa Mohamed ni mtu muungwana sana na anamwandalia chakula chochote anachojisikia,” anasema El Ataoui.

Mara zote ambazo unakuwa na Msuva simu namba moja kuita zaidi ni ya El Ataoui. Zaidi amekuwa akimpa moyo katika matukio mbalimbali ya ndani na nje ya uwanja. Katika pambano la ugenini dhidi ya Rapide Oued Zem ambalo nilishuhudia Msuva hakufunga tofauti na alivyopania na wakati mimi na El Ataoui tukirejea nyumbani kwa gari binafsi, huku Msuva akiwa katika basi la timu alimpigia simu kuelezea masikitiko yake kwa kutofunga.

“Unaona, huyu hapa Saimon amenipigia. Anajisikia vibaya kutofunga. Kila kitu ni lazima anipigie simu kuniambia jinsi ambavyo anajisikia. Akihisi kitu chochote lazima anipigie simu. Nimekwishazoea. Ndiye mchezaji ambaye niko naye karibu zaidi.” Pambano dhidi ya FUS Rabat, Kocha Taleb Abderrahim alimweka nje Msuva na wachezaji wengine wanne ambao huwa wanacheza kikosi cha kwanza. Lengo lake lilikuwa ni kuwapumzisha kutokana na kucheza mechi nyingi mfululizo. Alitaka kuwatumia katika pambano dhidi ya Wydad Casablanca wikiendi iliyopita.

“Si unaona. Kama leo usiku nitakuja nyumbani kwa Saimon na kumweleza vizuri kwa nini hajapangwa katika mechi hii. Najua atakuwa ameumia na sidhani kama atalielewa vyema pengo la kocha, hivyo nitakuja kuzungumza naye vizuri kabisa na ataelewa. Hii ni moja kati ya kazi zangu,”anasema

Kufika hapo najaribu kumdodosa El Ataoui kuhusu uwezekano wa Msuva kuondoka Morocco na kwenda kucheza soka la kulipwa barani Ulaya hasa ukingatia Morocco imepakana kwa karibu na Hispania.

El Ataoui anatoa jibu zuri ambalo kila shabiki wa Tanzania angependa kulisikia. Anazungumza nini kuhusu suala la Msuva kucheza soka la kulipwa? Je, ana mipango gani na Msuva? Kumbe pia kuna urafiki kati ya El Ataoui na wakala wa Mbwana Samatta? Fuatilia toleo la kesho.

Itaendelea