Hili tatizo la VIDAL Unalifahamu lakini? Cheki atakavyopona

Muktasari:

  • Taarifa za mtandao wa klabu hiyo pamoja na akaunti ya Twitter ya Vidal zinaeleza aliumia wakati akifanya mazoezi ya timu Jumapili iliyopita.

KIUNGO wa Bayern Munich, Arturo Vidal amethibitika kupata majeraha mapya ya goti na hivyo kuhitajika kufanyiwa upasuaji kwa ajili ya kutibu tatizo hilo.

Taarifa za mtandao wa klabu hiyo pamoja na akaunti ya Twitter ya Vidal zinaeleza aliumia wakati akifanya mazoezi ya timu Jumapili iliyopita.

Kocha wa Bayern Munich, Jupp Heynckes alisema hakuna aliyemchezea vibaya Vidal, bali aliteleza na kuanguka. Kocha huyo alifuatilia kwa karibu suala hilo ili kujua majeraha hayo yatamuweka kwa muda gani nje ya uwanja. Vidal tayari ameshatua jijini Augsburg, akisubiri kufanyiwa upasuaji wa matundu.

“Nimepokea simu ya Dk. Muller-Wohlfar, anasema kipimo cha picha cha MRI kimefanyika na imeonekana ungio la goti lake lina jeraha na kusababisha kukosa udhibiti.”

Tatizo hilo ndilo linazuia ungio la goti lake kushindwa kunyooka, atahitaji upasuaji mdogo wa matundu ujulikanao kama Anthroscopic Procedure na amehakikishiwa kuwa atakuwa nje kwa muda mfupi. Imeelezwa ataukosa mchezo wa nusu fainali ya Uefa kati ya Buyern Munich na Real Madrid, kutokuwepo kwake ni pigo kwa klabu yake na hivyo kutoa nafasi kubwa kwa Madrid kuibuka na ushindi. Aina ya majeraha na matibabu yake yanaondoa pia uwezekano wa kuwemo katika mechi zote za ligi zilizobakia.

Hii ni wiki mbaya kwa wanasoka wa Amerika ya Kusini, ambapo pia straika, Kun Aguero anayekipiga Manchester City anatarajia kukosa mechi zote za ligi zilizobakia kutokana na majeraha ya goti.

Leo nitawapa ufahamu juu ya upasuaji wa matundu wa kisasa wa magoti ujulikanao kama Anthroscopic Surgery ambao ndiyo njia rahisi katika uchunguzi na kutibu baadhi ya majeraha ya goti.

IKO HIVI

Huu ni upasuaji wa kisasa wa matundu madogo unaokoa damu kupotea wakati wa upasuaji hii ni kwa sababu kunahitaji uwazi mdogo tu kwa ajili ya kupenyeza kifaa tiba (anthroscope).

Matundu mawili hutobolewa na kuingiziwa kifaa chenye lenzi na taa inayomulika, lengo ni kuona kwa ufasaha vitu vyote vilivyomo ndani ya ungio la goti na pia kuvikuza vile vidogo vionekane vizuri.

Kifaa hicho huwa na ukubwa kama wa penseli huwa na mfumo maalumu wa kielektoniki na picha hukuzwa katika skrini kubwa hivyo kumwezesha daktari kuona vitu vilivyomo katika ungio, vizima na vyenye shida.

Katika ungio la goti kwa kifaa hiki tiba, daktari huweza kuona vitu vilivyomo katika ungio la goti ikiwamo mifupa, katileji, nyuzi za ligamenti na tendoni na kifupa cha goti.

Kifaa hicho kinamwezesha daktari kubaini ukubwa au aina ya jeraha na hivyo kuweza kutibu tatizo kuendana na muongozo sahihi wa tiba.

Unaweza kujiuliza ni kwa nini upasuaji huu unatumika? Kwa kawaida matatizo kama aliyopata Vidal ili kujua ukubwa na aina ya jeraha itakubidi kupata historia ya mgonjwa, uchunguzi wa jumla wa kimwili na ufanyaji wa vipimo mbalimbali ikiwamo picha ya X-ray.

Tumeona katika maelezo ya awali, Vidal alipigwa picha ya MRI ambayo nayo inatoa taswira nzuri juu ya vitu vilivyomo katika ungio lakini kwa uhakika zaidi kujua kilichomsibu mgonjwa wa majeraha ya goti ni upasuaji huu wa matundu pekee.

Kwa kutumia kifaa tiba cha Anthroscope daktari hufanya bainisho (diagnosis) la mwisho kwa uhakika na kujua kwa kina tatizo zima la majeraha ya ungio kuliko kwa kutumia upasuaji wa kawaida au picha ya X-ray.

Magonjwa au majeraha ya ungio la goti yanaweza kuambatana na kuvunjika mfupa, katileji, kujeruhi nyuzi za ligamenti na tendoni na tishu nyingine laini.

Wakati wa upasuaji wa anthroscopic daktari hubaini kirahisi matatizo kama haya yanayojitokeza mara kwa mara na kuyakabili. Moja ya faida kubwa ya upasuaji huu ni mgonjwa kwenda nyumbani ndani ya saa 24. Ukilinganisha na upasuaji wa goti wa kizamani mgonjwa huitaji kukaa siku 3-5 hospitalini.

Upasuaji huu kama ulivyo njia nyingine mgonjwa pia atahitaji kupewa dawa za usingizi au za ganzi au ya uti wa mgongo kukata hisia za maumivu eneo la chini ya mgongo katika eneo lilipo jeraha.

Pale upasuaji unapoisha vidonda vidogo vya matundu vyenye ukubwa kama kifungo cha shati huwekewa gozi maalumu na kisha hupelekwa chumba maalumu kwa ajili ya uangalizi wa muda.

Mgonjwa anaweza akapewa ama asipewe dawa za maumivu kisha kama daktari ataona hakuna tatizo mgonjwa anaweza kupewa ruhusa kurudi nyumbani.

Sitashaanga kusikia pia Vidal amefanyiwa upasuaji huu na kuruhusiwa kurudi nyumbani huku akipewa maelekezo maalumu kwa ajili ya uangalizi wa vijeraha vya vitundu vya upasuaji. Moja ya maelekezo ni aina gani za shughuli zakuepuka na mazoezi gani mepesi ufanye ili kusaidia kupona.

Wakati wa kurudi tena hospital kwa ajili ya ufuatiliaji daktari atakagua vitundu vya upasuaji na kuondosha nyuzi katika kijeraha hicho.

Baadaye mgonjwa akibainika amepona kabisa anaweza kuanzishiwa programu ili aweze kukitumia kiungo kilichopata majeraha kama ilivyokuwa awali kabla ya kuumia.

Ni kawaida pia katika upasuaji huu kukatokea mabadiliko katika aina ya upasuaji, mfano wakati wa upasuaji huu wa matundu, daktari anaweza kubaini tatizo ni kubwa hivyo kuhitaji upasuaji mkubwa.

Kutokana na alichokibaini anaweza kuamua kuendelea na upusuaji mkubwa siku hiyohiyo ukiwa katika usingizi au ganzi ama akapanga tarehe ya siku nyingine ya upasuaji.

Yako madhara machache ambayo huwa yanaweza kutokea kwa uchache sana ikiwamo uambikzi, buja la damu kuganda katika mishipa ya veini na jeraha kuvimba na kuvuja damu. Vilevile madhara mengine ni pamoja maumivu makali, kujeruhiwa kwa mishipa ya damu au fahamu na kuvunjika kwa kifaa tiba ndani ya kiungo kilichojeruhiwa.

Madhara haya yanatokea chini ya asilimia moja ya wagonjwa wote wanaofanyiwa upasuaji wa matundu na ndiyo maana upasuaji huu unaaminika kuwa ni salama.

Itahitaji wiki kadhaa kwa Vidal kurudi katika mazoezi.

Kwakuwa soka ni mchezo unaotumia nguvu nyingi, ndiyo maana haitakuwa rahisi Vidal kupona na kushiriki mchezo wa nusu fainali dhidi ya Real Madrid.