Hawa Watani wa Kariakoo wamefanya biashara kichaa

Muktasari:

  • Mechi ya kwanza Yanga walichapwa mabao 2-1 na Township Rollers pale Uwanja wa Taifa, saa 24 zilizofuata, Simba wakatoka sare ya mabao 2-2 na Al Masry ya Misri. Juzi wote wakabana wakatoka suluhu mbili tofauti ugenini. Kisayansi ya soka hapo kuna maana mbili. Kwanza kabisa inawezekana wenyeji wetu walipunguza kasi ya mchezo kwa sababu tayari kadri dakika zilivyosonga mbele ndivyo ambayo walikuwa wanalinda matokeo yao ya Dar es salaam kuliko kutafuta ushindi.

WATANI wa Kariakoo wamefanya biashara isiyo na faida. Wananikumbusha yule mgonjwa wa Muhimbili ambaye alipasuliwa kichwa wakati alikuwa na tatizo la mguu. Wangeweza kufanya kitu zaidi lakini hawakufanya.

Mechi ya kwanza Yanga walichapwa mabao 2-1 na Township Rollers pale Uwanja wa Taifa, saa 24 zilizofuata, Simba wakatoka sare ya mabao 2-2 na Al Masry ya Misri. Juzi wote wakabana wakatoka suluhu mbili tofauti ugenini. Kisayansi ya soka hapo kuna maana mbili. Kwanza kabisa inawezekana wenyeji wetu walipunguza kasi ya mchezo kwa sababu tayari kadri dakika zilivyosonga mbele ndivyo ambayo walikuwa wanalinda matokeo yao ya Dar es salaam kuliko kutafuta ushindi.

Lakini pia kuna uwezekano mkubwa kwamba Simba na Yanga walitumia mechi za awali kusoma upungufu na nguvu za adui. Ina maana kwamba walizijua zaidi timu pinzani baada ya kucheza nazo mechi za kwanza nyumbani.

Hii ina maana kwamba hawakutuma mashushushu wataalamu wa soka ambao wangeweza kusafiri kwenda Botswana na Misri kuzichunguza timu hizi. Niliwahi kuhojiwa sehemu nikaweka wazi kwamba wakati mashabiki wa Simba pamoja na viongozi wao wakipiga kelele kuhusu mshambuliaji mrefu wa Burkina Faso, Aristide Bance, huenda staa huyo asiwe mchezaji hatari kuliko wachezaji wengine wa Al Masry.

Hiki ndicho kilichotokea. Katika safu ya ushambuliaji ya Waarabu hao kulikuwa na watu ambao walionekana kuwa hatari kuliko Bance. Katika mechi ya kwanza Bance alianzia benchi na wakati anaingia tayari wageni walikuwa wameshafunga mabao mawili.

Tunahitaji kuzitazama na kuzisoma vema timu pinzani kabla hazijafika nchini hususani pale ambapo mechi za kwanza zinaanzia nyumbani. Simba na Yanga zimeondolewa kwa mabao manne ambayo wameyaruhusu kizembe uwanja wa Taifa.

Walijifunza kucheza na wageni wakiwa tayari ndani ya uwanja. Katika nchi za wenzetu, makocha au wasaidizi wanaoaminika katika kuusoma mchezo wangeweza kusafiri kwa ajili ya kwenda kuusoma mchezo ugenini kabla ya timu hizo hazijakutana.

Umakini ambao wameonyesha katika mechi za juzi walipaswa kuonyesha katika mechi za Uwanja wa Taifa. Mbaya zaidi ni pale ambapo mechi ya kwanza inachezwa katika uwanja wa nyumbani halafu mechi ya pili inachezwa uwanja wa ugenini.

Tatizo jingine ambalo limenichekesha kwa Simba na Yanga kutolewa katika michuano hii ni jinsi ambavyo hawana umakini sana katika masuala ya pesa. Wapo makini sana katika masuala ya kusaka ufalme baina yao kuliko kusaka pesa.

Nitakupa mfano mmoja. Wakati mechi ya Simba na Yanga inakaribia, klabu hizi zinakuwa makini. Zinasafiri kwenda kujificha. Timu moja unasikia inakwenda Pemba nyingine inakwenda Unguja. Wanachosaka ni ufalme baina yao lakini mwisho wa siku mapato yanayopatikana uwanjani yanawaacha wakiwa na shilingi 80 milioni.

Maandalizi yao ya mechi dhidi ya Township Rollers na Al Masry hayakuwa hivi. Walikuwepo hapa hapa mjini na wala hawakuwa na hofu sana na wapinzani wao. Kumbe hizi ni mechi ambazo kama wangejipanga sana wangeweza kufika robo fainali na kutwaa zaidi ya shilingi 200 milioni kila moja kwa kufikia hatua hiyo.

Hata hivyo kisaikolojia wachezaji wa Simba na Yanga wameendelea kuona kuwa mechi ya Simba na Yanga ni muhimu kuliko mechi za CAF. Hata mabosi wetu wameendelea kuona hivyo. Simba walidiriki kwenda Morogoro kujiandaa kucheza na Singida United wakati wala hawakuona umuhimu wa kwenda popote kujiandaa kucheza na Al Masry. Hii ndio biashara kichaa.

Pamoja na yote haya, mwisho wa siku timu zetu zinahitaji kujiimarisha zaidi. Zimeondolewa na klabu ambazo ni bora. Naweza kuwasifu zaidi Simba kwa sababu walicheza na timu ambayo inatoka katika nchi iliyotupita sana kisoka lakini bado wametoka sare mbili.

Yanga wajipime na kujiridhisha. Wameshuka sana. Bado naamini kwamba miezi 15 iliyopita Yanga wangeweza kuitoa Township bila ya shida. Yanga yenye Donald Ngoma, Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Simon Msuva, Amissi Tambwe, Juma Abdul, Obrey Chirwa na wengineo ingeweza kuitoa Township.

Hapo hapo ninaamini kwamba kama Simba wangepambana na Township Rollers wangeweza pia kuwatoa. Yanga wanahitaji suluhisho la matatizo yao baada ya kuondoka kwa tajiri wao Yusuf Manji. Ina wachezaji wengi wa kawaida sana ambao miezi 15 nyuma walikuwa hawastahili kuvaa jezi ya Yanga.

Wanahitaji suluhisho jipya kwa sababu walijiweka katika kiwango cha juu ambacho kilikuwa kinatia matumaini ya kufanya vizuri katika michuano ya Afrika, kwa sasa wamerudi chini na chini. Hata huko katika michuano ya Kombe la Shirikisho walikokwenda sioni kama wanaweza kufanya maajabu yoyote.

Tukiachana na hilo, watani wa Kariakoo wamefanya biashara kichaa katika mechi hizi mbili. Wanahitaji kujichunguza walikosea wapi. Hawajakosea sehemu kubwa sana kama matokeo yanavyoonyesha.