Kutamka majina ya wachezaji hawa nenda kwanza kozi

SHERIA za mpira zinahitaji jina la mchezaji liwe limeandikwa kwenye jezi sehemu ya mgongoni hasa kwa mechi za kiushindani. Lakini, shida inakuja kwenye baadhi ya majina ni magumu mno kuyatamka na watangazaji, wachambuzi na hata mashabiki wamekuwa wakipata shida kuyatamka na kuishia kutaja tu namba zilizopo kwenye jezi wanazova wachezaji hao.

Utasikia tu yule mchezaji namba 9 au yule mwenye namba 15, hiyo yote ni kwa sababu ya ugumu wa kuyatamka majina yao. Hawa ndio wanasoka waliopo kwa sasa ambao majina yao kuyatamka ni pasua kichwa kweli kweli.

7.Pierre-Emerick Aubameyang- Arsenal

Straika wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang hakuna ubishi ni mmoja wa wachezaji wenye vipaji vikubwa sana waliopo Ligi Kuu England kwa sasa. Tangu alipojiunga na timu hiyo Januari amefunga mabao 10 katika mechi 14 alizocheza kwenye michuano tofauti. Kocha mpya, Unai Emery hakika atahitaji kukijenga kikosi chake kipya kumzunguka mshambuliaji huyo. Lakini, shida itakayomkali kocha huyo ni kutamka jina lake jinsi lilivyorefu hivyo ni pasua kichwa.

6.Gylfi Sigurðsson- Everton

Kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Iceland, Gylfi Sigurðsson anakipiga Ligi Kuu England katika kikosi cha Everton. Ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa sana wa kupiga mipira ya adhabu na kufunga mabao yake ya umbali wa mita 40, hivyo mashabiki watakaokwenda Russia watakwenda kushuhudia makali yake na zile pasi zake za mwisho matata. Lakini, shida itakuja kwenye kulitamka jina lake pale atakapofanya mambo uwanjani.

5.Reza Ghoochannejhad- Heerenveen

Staa wa kimataifa wa Iran, Reza Ghoochannejhad Nournia ni straika anayekipiga Heerenveen. Aliwahi pia kuichezea Charlton Athletics ya England. Atakuwapo Russia na hakika jina lake litakuwa mtihani mzito kwa watangazaji wa mechi za fainali hizo, walau kidogo jina lake la kwanza.

4.Wojciech Szczesny- Juventus

Kipa wa Juventus, Wojciech Szczesny si jina geni sana kwenye soka kwani aliwahi kuichezea Arsenal na yupo pia kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Poland. Ni shughuli pevu kulitamka jina lake na hakika hilo lilikuwa likiwapa shida mashabiki wa Arsenal na hata Juventus anakocheza kwa sasa na wengi wao wamekuwa wakijaribu kutamka jina la pili, lakini hilo la kwanza ni shughuli nzito.

3.Kolbeinn Sigþórsson- Nantes

Straika wa kimataifa wa Iceland, Kolbeinn Sigþórsson anacheza soka Ligi Kuu ya Ufaransa akikitumikia kikosi cha Nantes. Ni kazi ngumu kweli kweli kutamka jina lake jambo ambalo hata watangazaji wamekuwa kwenye shughuli pevu wanapotangaza mechi za Nantes au Iceland.

2.Sokratis Papastathopoulos- Borussia Dortmund

Sokratis Papastathopoulos kwa vyovyote vile atakuwa ni mchezaji wa kutoka Ugiriki kutokana na ubini wake. Anakipiga kwenye kikosi cha Borussia Dortmund huko kwenye Bundesliga akiwa beki wa kati na kwa mujibu wa taarifa anakaribia kuhamia Arsenal. Hakika jina lake litawavunja ulimi mashabiki wa Arsenal kulitamka, ni mtihani wa kwanza huko Emirates.

1.Jakub Blaszczykowski- Wolfsburg

Staa wa kimataifa wa Poland, Jakub “Kuba” Blaszczykowski anacheza winga kwenye kikosi cha VfL Wolfsburg ya Ujerumani. Mchezaji huyo alipata mafanikio makubwa sana wakati alipokuwa Borussia Dortmund iliyokuwa chini ya Jurgen Klopp. Alikuwa kipenzi cha mashabiki, lakini shida ilikuwa sehemu moja tu, kulitamka jina lake.