HAPA KAZI TU: Kocha Pep Guardiola si mtu wa mchezo akiwa mazoezini - 129

Muktasari:

“Baada ya hapo nitawataka kudhihirisha nguvu zao na si kubweteka, nawapa muda mfupi mno wa kuvuta pumzi na kujiweka sawa, lengo ni kuhakikisha wanafanya mazoezi matatu kwa mkupuo, kila moja kwa sekunde 30 hadi 40,’’ anasema Buenaventura.

KATIKA toleo lililopita kwenye kitabu cha Pep Confidential, tuliona namna ambavyo Kocha Pep Guardiola anaendesha mazoezi akisaidiana na wasaidizi wake akiwamo Lorenzo Buenaventura katika utaratibu maalumu wenye lengo la kuhakikisha kila mchezaji anakuwa na utimamu wa maeneo yote muhimu. Endelea…

“Baada ya hapo nitawataka kudhihirisha nguvu zao na si kubweteka, nawapa muda mfupi mno wa kuvuta pumzi na kujiweka sawa, lengo ni kuhakikisha wanafanya mazoezi matatu kwa mkupuo, kila moja kwa sekunde 30 hadi 40,’’ anasema Buenaventura.

Kwa kufanya hivyo unahakikisha mchezaji anakuwa katika kiwango kinachotakiwa kwa wakati wote, anakuwa kiwango cha juu. Hadi hapo wachezaji walikuwa wamemaliza utaratibu wote kwa zoezi la mwisho la kupiga mashuti 18 golini, kwa wakati wote ni kutafuta uwiano katika nguvu za mwili na mbinu za kiuchezaji.

Zoezi zima pia lina malengo mawili, kwanza ni kuwafanya wachezaji wawe mahiri kwenye maeneo yao ya kiuchezaji, jambo muhimu katika utaratibu wa Pep. Katika kila mita 20 kuna timu mbili, kila timu ina wachezaji saba.

Pia kunakuwa na wachezaji wanne ambao wanacheza kote kote, hawa wanaweza kuiunganisha timu yoyote na mpira. Kinachotakiwa kufanyika hapo ni kwa kila timu kupeana pasi nyingi kadri iwezekanavyo bila mpira kunyang’anywa na timu nyingine.

Yoyote anayekuwa na mpira anajaribu kufungua uwanja, pamoja na udogo wa eneo wakati huo huo timu pinzani inajitahidi kukaba kwa nguvu zote, kila mchezaji anatakiwa kufahamu namna ya kujiweka ili apewe mpira ataunasa vipi kwanza kabla ya kutoa pasi, aende wapi na vipi pasi zitolewe kwa haraka ingawa kwa kawaida hili linafanyika baada ya kuugusa mpira mara moja.

Ni aina ya zoezi ambalo linahitaji umakini wa hali ya juu, uwe makini na mwenye mbinu, uwe mwenye malengo katika utoaji pasi na umiliki wa mpira kwa kila hatua.

Kuna wakati Pep anawaambia baadhi ya wachezaji mfano kina Thiago, Schweinsteiger, Kroos na Lahm kuugusa mpira mara mbili wakati wengine wote wanatakiwa kutoa pasi kwa kuugusa mara moja, hali hiyo bado inalifanya zoezi kuwa pana na lenye mambo mengi.

Baadaye Pep anakuja na jambo jingine, anayataka makundi haya matatu ya wachezaji kutumia dakika mbili kufanya mazoezi mepesi ya viungo kujiweka fiti, wakati zoezi hili likiendelea hakuna muda wa kupumzika, wakati wote Pep anakuwa hapo kuwasahihisha wanapokosea.

Hakuna ubishi kilichokuwa kikishuhudiwa hapo ni kitu muhimu na chenye mantiki kwa wachezaji, ni kitu kikubwa ambacho kilifanyiwa kazi kwenye eneo dogo. Hakukuwa na hali ya kutabasamu, kupumzika au masihara ya aina yoyote, ni kazi tu na umakini wa kiwango cha juu.

Wachezaji walikuwa wakitafuta ubora, namna nzuri ya kwenda na mpira, kujipanga eneo sahihi kwa mchezaji binafsi pamoja na timu na baada ya hapo kulikuwa na kitu ambacho Pep alikibatiza jina la tac tac.

Ni mlio au mwangwi uliosikika Sabener Strasse unaosikika wakati mpira ukienda huku na kule, sit u kwa umakini bali kwa kasi, mbele na nyuma katika sekunde chache ukiwahusisha wachezaji kina Lahm na Thiago au Kroos na Thiago, pasi mbili katika sekunde moja lakini kwa kurudiarudia.

Hatimaye ulifika wakati wa kufanya zoezi la mwisho la siku, washambuliaji waliachiwa na kuanza kazi ya kuwasumbua makipa, Neuer na Starke kwa mashuti, ni zoezi la dakika 20. Kwa kawaida Muller, Mandzukic na Kroos wanahusika katika zoezi hili.

Mwingine anayeungana nao ni Pizarro lakini zaidi ya huyo pia alikuwapo Robben ambaye hana kawaida ya kufanya zoezi la kupiga mashuti kwenye goli, lakini aliamua kuungana na kundi hilo.

Kocha pia amepanga kazi ya kufanya na mabeki, kazi ya kukabiliana na mashambulizi ya kushitukiza, Rafinha, Van Buyten, Contento na Alaba walijipanga kwa kazi hiyo.

Pia katika kundi hilo alikuwapo Javi Martinez, Hojbjerg na wachezaji wanne wa timu ya vijana wa safu ya ushambuliaji waliokuwa wakipeana pasi ili kuwatoka mabeki wa kati na pembeni na hatimaye kufikisha pasi na krosi.

Itaendelea Jumanne ijayo…