Wakitua England Patanoga

Tuesday May 15 2018

 

LONDONENGLAND


ASIKWAMBIE mtu, Ligi Kuu England na makali yake yote itanoga zaidi kama itanasa mastaa hawa ambao wanatamba huko kwingine.

Si kama kwenye ligi hiyo hakuna wachezaji wa maana, lakini kama mastaa hao watatua, basi watafanya mambo kuwa matamu zaidi.

Toni Kroos (Real Madrid)

Kiungo wa kati, Toni Kroos ni mmoja kati ya wachezaji matata ambao staili ya soka lao limewafanya kujikusanyia mashabiki wengi duniani. Mjerumani huyo panga pangua amekuwa kwenye kikosi cha kwanza cha Real Madrid na jambo hilo linatoa uhakika hawezi kuja kuvurunda akitua Ligi Kuu England.

Hakuna ubishi, mashabiki watamhitaji kumuona akicheza moja ya timu zilizopo Ligi Kuu England msimu ujao. Kuna wakati Manchester United ilihusishwa na huduma yake na huenda akanaswa kurithi mikoba ya Michael Carrick.

Neymar (PSG)

Supastaa wa Kibrazili, Neymar ni gumzo Ulaya. Baada ya kutua kwa pesa nyingi Paris Saint-Germain akitoka Barcelona, mwaka mmoja tu baadaye, anahusishwa na mpango wa kuachana na wababe hao wa Ufaransa. Jina la staa huyo linahusishwa na kurejea La Liga, huko Real Madrid. Lakini, wiki za karibuni, Man United imeripotiwa kuhitaji huduma yake na ipo tayari kuvunja benki kunasa saini ya mchezaji huyo. Hakuna ubishi, Neymar ni aina ya wachezaji ambao mashabiki wa Ligi Kuu England watatamani sana kuwaona kwenye ligi hiyo.

Lionel Messi (Barcelona)

Ngumu kufikiria jambo hilo kutokea Ligi Kuu England, supastaa Lionel Messi kwenda kucheza moja ya timu zilizopo kwenye ligi hiyo.

Manchester City kuna wakati ilifikiria mpango wa kunasa huduma ya mchezaji huyo, hasa baada ya ujio wa Kocha Pep Guardiola, Etihad. Baada ya kutamba kwa muda mrefu kwenye La Liga, kuna wanaoamini Messi huenda asingekuwa na makali hayo angekuwa England na ndiyo maana mashabiki wanatamani sana kumuona Muargentina huyo akiwa kwenye viwanja vya ligi ya England kila wikiendi, kuona kama kweli atakuwa na makali yake na kutesa kama anavyotesa huko kwenye La Liga.

Robert Lewandowski (Bayern Munich)

Ripoti zinadai wandowski huenda akaachana na Bayern Munich mwishoni mwa msimu huu. Real Madrid inatajwa kwenye mpango wa kumnasa, lakini huduma yake inahitajika sana kwenye Ligi Kuu England.

Man United inahitaji straika mwingine wa kusaidiana na Romaleu Lukaku. ManCity inahitaji pia straika wa kusaidiana na kina Gabriel Jesus. Kocha Liverpool, Jurgen Klopp naye anahitaji mshambuliaji wa kati na jambo hilo linamfanya Lewandowski kuwa na wigo mpana wa kuchagua timu zinazohitaji saini yake.

Paulo Dybala (Juventus)

Kwenye kikosi cha Juventus, Dybala ameonyesha ubora wake na kumfanya atambulike karibu katika kila kona ya dunia.

Lakini, hakuna ubishi kuichezea Juventus si sawa na kuichezea Manchester United, unapokuwa kwenye klabu hiyo ya Ligi Kuu England umaarufu wako unaongezeka maradufu. Kutokana na hilo, Dybala ni mmoja kati ya wachezaji ambao hakika mashabiki wangetamani kuwaona wakifanya mambo yao kwenye Ligi Kuu England kwa kujiunga na moja ya timu za ligi hiyo, hasa vigogo ama Man City au Man United. Hata Liverpool au Arsenal, timu ambazo zinaonekana kuwa na mashabiki wengi kwenye kona tofauti za duniani hii.

Akienda Chelsea nako si haba, atakwenda kuunda kikosi kimoja na mkali Eden Hazard.

Edinson Cavani (PSG)

Kunasa huduma ya Cavani ni kujihakikishia mabao. Supastaa huyo wa Paris Saint-Germain amekuwa kwenye kiwango bora kabisa msimu huu na kutupia tu mipira wavuni.

Tangu Zlatan Ibrahimovic alipoondoka kwenye kikosi cha PSG, Cavani ameibuka na kuwa shujaa wa kikosi hicho. Kuna wakati Cavani alihusishwa na mpango wa kutua Ligi Kuu England ambapo Man United na Arsenal zilionyesha dhamira ya kuhitaji huduma yake na hakika ingekuwa burudani ya kutosha kwa mashabiki wa Ligi Kuu England kama straika huyo angekuwa kwenye moja ya vikosi vya timu hizo.

Hata hivyo, furaha hiyo itaendelea kuwapo kama mwishoni mwa msimu huu, Cavani atakubali kwenda kujiunga na moja kati ya vigogo vya Ligi Kuu England.

Antoine Griezmann (Atletico)

Kama kinachoelezwa ni kweli basi, supastaa huyo wa Ufaransa anaripotiwa mwishoni mwa msimu huu ataachana na Atletico Madrid na kutikia Barcelona.

Kumekuwa na ripoti pia kwamba Barcelona inafanya mpango wa kumwondoa Luis Suarez kwenye kikosi chake ili kumvuta Griezmann. Lakini, miezi si mingi sana imepita, staa huyo jina lake lilihusishwa na mpango wa kwenda kujiunga na Man United na kwamba dili hilo bado halijakufa kwa sababu dirisha lijalo halijafunguliwa, Kocha Jose Mourinho anaweza kutazama upya mpango wa kumsajili staa huyo.

Kuna wakati Chelsea na Man City nazo zilihusishwa na mchezaji huyo, huku ujio wake kwenye moja ya vikosi vya Ligi Kuu England utaleta burudani ya kutosha kwa sababu utafanya ligi kuwa na utamu wa aina yake.

Karim Benzema (Real Madrid)

Kwa muda mrefu sana, Karim Benzema amekuwa mmoja kati ya wachezaji ambao mashabiki wangependa sana kuwaona kwenye Ligi Kuu England.

Kuna wakati Arsenal ilihitaji sana huduma yake na katika kipindi hiki ambacho Real Madrid imejipanga kujitengeneza upya, Benzema anaonekana ni mmoja kati ya wachezaji ambao watafunguliwa mlango wa kutokea kwenye kikosi hicho. Hakuna ubishi, Benzema bado ni mchezaji anayeweza kufanya mambo makubwa ndani ya uwanja na huduma yake kama itanaswa na moja ya timu za Ligi Kuu England hasa Arsenal au Liverpool na hata Chelsea kitakuwa kitu kizuri kwa mashabiki wa Ligi Kuu England.

Kylian Mbappe (PSG)

Ligi Kuu England imekuwa na makinda matata kabisa kama vile Anthony Martial, Leroy Sane, Gabriel Jesus, Marcus Rashford na wengine kibao. Kitakuwa kitu maana na mvuto mkubwa kwa mashabiki wa ligi hiyo kama Mbappe naye atakuwa kwenye orodha ya makinda hao watakaokuwa wakionyesha makali yao na kushindana kwenye Ligi Kuu England.

Liverpool, Manchester City na Arsenal zilionyesha dhamira ya kumsajili kwenye dirisha lililopita kabla ya Mfaransa huyo kuamua kwenda kujiunga na PSG kwa mkopo akitokea Monaco.

Kwa kile alichokifanya akiwa Monaco na alichokwenda kuendelea kukifanya PSG, Mbappe ni mmoja kati ya wachezaji ambao mashabiki wa Ligi Kuu England wangekuwa kwenye furaha kubwa kama wangemuona akicheza kwenye ligi hiyo, kwa sababu angefanya kuwapo na upinzani mkali kwa kila wiki.

Sergio Ramos (Real Madrid)

Kama kuna beki wa kati ambaye hakuna timu yeyote ambayo isingependa kuwa na huduma yake ndani ya uwanja basi, ni Sergio Ramos wa Real Madrid.

Beki huyu ni moto kwelikweli na wakati mwingine amekuwa akifunga mabao muhimu kusaidia timu yake kupata ushindi.

Kama kuna mchezaji ambaye Liverpool itapaswa kumwogopa watakapochuana na Real Madrid kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Mei 26, basi ni beki huyo kutokana na uwezo wake wa kukaba na wakati huohuo kwenda mbele kushambulia. Kuna wakati Ramos alihusishwa na Man United na jambo hilo liliwafanya mashabiki wa timu hiyo kufurahia sana kabla ya dili lenyewe kukwama. Bado kitakuwa kitu chenye kuvutia kama Ramos atakwenda kujiunga na moja ya timu za Ligi Kuu England msimu ujao.