Sanchez: Nina njaa kuipa mataji Man United

Muktasari:

Pia alisema ana deni la kuwalipa mashabiki wa klabu hiyo baada ya kupewa jezi namba saba inayovaliwa na wachezaji nyota Man United.

London, England. Mshambuliaji mpya wa Manchester United, Alexis Sanchez amesema ana njaa ya kuipa mataji mengi klabu hiyo.

Pia alisema ana deni la kuwalipa mashabiki wa klabu hiyo baada ya kupewa jezi namba saba inayovaliwa na wachezaji nyota Man United.

Baadhi ya wachezaji waliowahi kuvaa jezi hiyo maalumu ni George Best, Eric Cantona, David Beckham na Cristiano Ronaldo.

Sanchez alitoa kauli hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kuzungumza na televisheni ya Man United muda mfupi baada ya kufaulu vipimo vya afya.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Chile, alidokeza tangu akiwa mdogo alikuwa na ndoto ya kucheza Man United kwa kuwa ni klabu aliyokuwa akiipenda.

“Sisemi hivi kwasababu nimejiunga na klabu hii, tangu nikiwa mdogo ndoto yangu ilikuwa kucheza Manchester United,” alisema Sanchez.

Mshambuliaji huyo alisema anatarajia kuifanyia makubwa Man United katika mashindano mbalimbali kwa kuwa ana uwezo wa kucheza nafasi zote za ushambuliaji.

Alisema anajua mashabiki wa klabu hiyo wanataka mataji, hivyo atacheza kwa juhudi kubwa kuhakikisha anawapa raha.

Sanchez alisema ni fahari kwake kucheza katika klabu kubwa iliyozungukwa na wachezaji mahiri akitolea mfano wa kipa David de Gea, aliyemtaja ndiye bora duniani.

‘Nitakuwa na faraja nitakapotambulishwa rasmi kwa wachezaji wenzangu, ingawa tunafahamiana uwanjani lakini sikuwa na rafiki Man United,”alisema mchezaji huyo.

Mchezaji huyo anatarajiwa kuanza kuvaa uzi wa Man United siku chache zijazo baada ya jana kuanza mazoezi rasmi kwenye Uwanja wa Carrington kujiandaa na mechi.