Ronaldo: Real Madrid ndio basi tena!

Muktasari:

Dili la Ronaldo kwenda Juventus ni mambo ya pesa tu. Wakati ikiripotiwa kwamba dili kale limegharimu Pauni 105 milioni kutoka Bernabeu kwenda Turin, lakini kinachoelezwa ni kwamba Ronaldo hadi anavua jezi za Los Blancos na kuvaa za Juventus, basi hesabu za mkwanja uliotumika unazidi Pauni 300 milioni.

TURIN, ITALIA. CRISTIANO Ronaldo amesema hivi, umefika wakati wake wa kuihama Real Madrid na kwenda Juventus.

Lakini, asikwambie mtu. Dili la Ronaldo kwenda Juventus ni mambo ya pesa tu. Wakati ikiripotiwa kwamba dili kale limegharimu Pauni 105 milioni kutoka Bernabeu kwenda Turin, lakini kinachoelezwa ni kwamba Ronaldo hadi anavua jezi za Los Blancos na kuvaa za Juventus, basi hesabu za mkwanja uliotumika unazidi Pauni 300 milioni.

Unaambiwa hivi, wakala wa Ronaldo, Jorge Mendes kwanza ameweka chake mfukoni, Pauni 10.6 milioni.

Manchester United wao wamevuta mgawo wao wa Pauni 4.4 milioni baada ya kushuhudia dili la mchezaji huyo likizidi Pauni 100 milioni.

Mshahara wa Ronaldo unaripotiwa kuwa ni Pauni 26.6 milioni kwa mwaka na amesaini mkataba wa miaka minne, hivyo hadi anafika tamati ya mkataba huo atakuwa ameweka mfuko Pauni 212 milioni.

Fiat ndio wanaoripotiwa kwamba watakuwa wakilipa mshahara wa sta huyo, Pauni 500,000 kwa wiki.

Kutokana namna anavyopiga pesa, Ronaldo ameripotiwa kutimia akili nyingi sana katika kulibamba dili hilo la Juventus. Akiwa na umri wa miaka 33, Ronaldo analipwa 70,000 milioni kwa siku.

Kiwango hicho cha pesa anawazidi mastaa kibao kwenye Ligi Kuu England, akiwamo Danny Welbeck wa Arsenal anayesubiria kiwango kama hicho kwa wiki, wakati mwenzake analipwa kwa siku moja, yani saa 24.

Real Madrid, ambao wanaripotiwa kusaka huduma ya mrithi wake huko Bernabeu, wamefanya dili la maana kwani wao walimsajili Ronaldo kwa Pauni 80 milioni mwaka 2009, lakini akiwa na umri wa miaka 33, miaka tisa baadaye, wanamuuza kwa Pauni 105 milioni. Dili la akili.

Kwenye kikosi cha Madrid, Ronaldo amefunga mabao 451. Mabao yake yote ni 659, matano alifunga akiwa na Sporting Lisbon, 118 akiwa na Man United,  451 akiwa na Real Madrid na 85 akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya Ureno.