Rashford kama Zlatan Man United

Tuesday August 7 2018

 

JOSE Mourinho amewaziba midomo wachambuzi wa soka wanamponda kuwa hampi kinda wake, Marcus Rashford muda wa kutosha uwanjani ili kuonyesha na kukuza kiwango chake.

Lakini katika kuonyesha kuwa anawajali vijana, Mreno huyo ameamua kumkabidhi Rashford jezi namba 10 ambayo imekuwa ikitumiwa na mastaa wakubwa ndani ya kikosi hicho.

Awali, Rashford alikuwa akivaa jezi namba 19, lakini sasa amepewa namba 10 iliyokuwa ikitumiwa na mastaa kama Mark Hughes, Teddy Sheringham, Ruud van Nistelrooy, Wayne Rooney na mwisho alikuwa Zlatan Ibrahimovic.

Kwa mara ya kwanza, Rashford alivaa jezi hiyo kwenye mchezo wa kirafiki wa juzi Jumapili usiku dhidi ya Bayern Munich, ambapo ni mara ya pili kubadilishiwa jezi chini ya Mourinho.

Wakati akipandishwa kwenye kikosi cha wakubwa, kinda huyo alikuwa akivaa jezi namba 39.

Kwa kupewa jezi namba hiyo, ni wazi Rashford ameanza kuaminiwa kwani jezi hiyo ni moja kati ya namba za heshima kwenye kikosi cha United.

“Ni rasmi sasa, Marcus Rashford ndio mmiliki wa jezi namba 10 wa Manchester United,” mtandao wa United uliandika.

Ibrahimovic alianza kutumia jezi namba 10 baada ya kuondoka kwa Rooney, ambaye aliitumia kwa miaka kadhaa na kuitendea haki. Kabla ya hapo Zlatan alikuwa akitumia jezi namba 9, ambayo sasa inavaliwa kwa Romelu Lukaku.