Pogba katoswa unahodha Man U

Muktasari:

Kulikuwa na mipango ya kumfanya Paul Pogba kuwa nahodha wa timu hiyo hasa baada ya kuisaidia Ufaransa kubeba ubingwa wa Kombe la Dunia 2018 huko Russia, lakini Mourinho amekuwa na mtazamo tofauti.

KOCHA wa Manchester United, Jose Mourinho amefichua Antonio Valencia ndiye atakayekuwa nahodha wake kwa msimu ujao.

Michael Carrick alikuwa nahodha wa timu hiyo kwa msimu uliopita, licha ya kwamba hakupata nafasi kubwa ya kucheza na kitambaa cha unahodha muda wote kilikuwa kwenye mkono wa Valencia.

Kulikuwa na mipango ya kumfanya Paul Pogba kuwa nahodha wa timu hiyo hasa baada ya kuisaidia Ufaransa kubeba ubingwa wa Kombe la Dunia 2018 huko Russia, lakini Mourinho amekuwa na mtazamo tofauti.

Kwenye orodha yake Mourinho, Pogba hayupo kabisa kwani alisema manahodha wake wa msimu ujao ni Valencia, Ashley Young, Ander Herrera na Juan Mata.

Mourinho alisema: “Valencia alikuwa nahodha wa msimu uliopita na nadhani ataendelea kuwa hivyo na kama hatacheza basi tutaangalia itakavyokuwa. Itategemea nani yupo uwanjani, kama ni Chris Smalling, Ashley Young, Ander Herrera au Juan Mata.

Pogba alidaiwa kuwapa hamasa Ufaransa kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Croatia na kushinda mechi hiyo kwa mabao 4-2 na Mourinho aliongeza.

“Kama wote watakuwa uwanjani basi hapo tutakuwa na machaguo ya kutosha.

“Nemanja Matic ana vigezo vyote, lakini aliwasili Man United mwaka mmoja tu uliopita. Mimi sijali kuhusu nahodha, ninachojali ni kuwa na viongozi kwenye vyumba vya kubadilishia. Kitambaa kina maana hiyo hiyo ilivyo.”