Pogba aingia anga za PSG

Muktasari:

Kipindi cha hivi karibuni uhusiano wa Pogba na Mourinho umeyumba kutokana na supastaa huyo wa Kifaransa kudaiwa kucheza chini ya kiwango na sasa huenda akawekwa sokoni.

Paris, Ufaransa. MATAJIRI wa Jiji la Paris, Paris Saint Germain (PSG) imeanza mchakato wa kusaka saini ya kiungo ghali wa Manchester United, Paul Pogba, ambaye kwa sasa anapitia kipindi kigumu chini ya Jose Mourinho pale Old Trafford.

Kipindi cha hivi karibuni uhusiano wa Pogba na Mourinho umeyumba kutokana na supastaa huyo wa Kifaransa kudaiwa kucheza chini ya kiwango na sasa huenda akawekwa sokoni.

Kwenye mechi ya kipigo cha bao 1-0 dhidi ya West Bromwich Albion, Pogba alitolewa uwanjani na nafasi yake kuchukuliwa na Anthony Martial, ambaye naye yuko njiapanda klabuni hapo kutokana na kugomea kusaini mkataba mpya.

Hata hivyo, mgogoro wa Pogba na Mourinho umekwenda mbali zaidi kiasi cha kumuibua wakala wa kiungo huyo, Mino Raiola ambaye ameweka bayana kwamba, mteja wake anaweza kuondoka Man United.

Mbali na Mourinho, wachambuzi mbalimbali wa soka nchini England, wanamponda Pogba kwa kiwango cha chini na kutowajibika uwanjani licha ya kuwa ni mchezaji ghali.