Ozil, Kosciely wakwaa unahodha Arsenal

Muktasari:

  • Aidha kutokana na nahodha huyo kutoingia dimbani hivi karibuni, Kocha huyo amewateua manahodha wanne wasaidizi akiwemo kiungo nyota wa Ujerumani Mesut Ozil.

London, England. Kocha mpya wa Arsenal, Unai Emery amemchagua Laurent Koscielny kuwa nahodha wake wa kwanza tangu atue Emirates, licha ya kuwa mlinzi huyo ni majeruhi atakayekaa nje kwa kipindi kirefu.

Aidha kutokana na nahodha huyo kutoingia dimbani hivi karibuni, Kocha huyo amewateua manahodha wanne wasaidizi akiwemo kiungo nyota wa Ujerumani Mesut Ozil.

Mara baada ya kutambulishwa Emery alisema atakuwa na manahodha watano ambao atakuwa akijadiliana nao katika masuala kadhaa yanayowahusu wachezaji na timu kwa ujumla.

Alibainisha kuwa Koscielny atakuwa nje hadi Desemba kutokana na kuwa majeruhi kutokana na upasuaji wa mshipa wa kisigino.

Ni kutokana na hilo ndio maana akaamua kuwateua wasaidizi wake miongoni mwa wale wenye uhakika wa kuanza katika mechi mbali mbali ambao ni, kipa Petr Cech, viungo Aaron Ramsey, Ozil na Granit Xhaka.

"Asubuhi hii ‘jana’ nimewateua manahodha wasaidizi wa timu nahodha mkuu ni Koscielny, atakuwa na wasaidizi wanne ambao ni Petr Cech, Aaron Ramsey, Mesut Ozil na Granit Xhaka,” alisema Emery.

Arsenal leo watashuka dimbani kumenyana na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Manchester City, katika mechi ya kwanza ya msimu huu.

Koscielny alikuwa nahodha msaidizi msimu uliopita wakati nahodha mkuu akiwa Per Mertesacker na Cech, Ramsey, Ozil na Xhaka kila mmoja aliwahi kuvaa kitambaa cha unahodha katika mechi za Arsenal msimu uliopita.