Mourinho haamini kama Pogba anaondoka

Muktasari:

Pogba amezidi kuufanya uvumi wa kuondoka kushika kasi zaidi baada ya wiki iliyopita kushindwa kukanusha kama anaweza kuondoka huko Old Trafford wakati wa usajili wa Januari. Lakini, Mourinho haamini kama kweli Pogba anataka kuondoka.

JOSE Mourinho amesema haamini kama kweli Paul Pogba anataka kuihama Manchester United kwa sababu kiungo huyo hajawahi kupeleka maombi ya kutaka kuondoka.

Barcelona waliripotiwa kumtaka kiungo huyo baada ya kudaiwa anataka kuihama Man United na hilo wanaweza kulifanya kwenye dirisha la Januari kutokana na mchezaji huyo kutokuwa na maelewano mazuri na kocha wake, Mourinho.

Pogba amezidi kuufanya uvumi wa kuondoka kushika kasi zaidi baada ya wiki iliyopita kushindwa kukanusha kama anaweza kuondoka huko Old Trafford wakati wa usajili wa Januari. Lakini, Mourinho haamini kama kweli Pogba anataka kuondoka.

“Paul amerudi kutoka kwenye Kombe la Dunia wiki moja kabla ya Ligi Kuu England kuanza. Tumekuwa pamoja kwa miezi miwili sasa na kamwe hajawahi kuniambia anataka kuondoka,” alisema Mourinho.

“Mimi najibu kile kilichokuwa cha kweli, siwezi kujibu kutokana na nilichosoma. Sina huo uhusiano wa moja kwa moja na watu wanaoandika mambo yao. Mimi nina uhusiano wa moja kwa moja na wachezaji, si Paul peke yake, bali ni wachezaji wengi. Yeye hajawahi kuniambia anataka kuondoka.”

Mkataba wa sasa wa Pogba unafikia tamati 2021, lakini Man United ipo kwenye hatari ya kuwapoteza mastaa wake kibao akiwamo Luke Shaw, Juan Mata na Ander Herrera kutokana na mikataba yao kufika tamati mwisho wa msimu huu.