Mourinho ana vichwa vitatu matata mezani

HII inaitwa biashara asubuhi, jioni unafunga hesabu. Kocha Jose Mourinho ameanza mapema kabisa mchakato wa kuwanasa mastaa anaowataka watue kwenye kikosi chake cha Manchester United ili kukifanya kuwa moto kwa msimu ujao.

Mourinho amegundua kuwapo na changamoto kwenye mabeki wa kati katika kikosi chake na hivyo ameanza kuzungumza na Tottenham Hotspur juu ya beki wa Kibelgiji, Toby Alderweireld.

Lakini Mreno huyo ameonekana kuweka nguvu pia kwenye kumsajili winga wa Chelsea, Mbrazili, Willian ili kuongeza nguvu katika kikosi hicho cha Old Trafford baada ya makinda kama Anthony Martial kushindwa kufanya mambo ya maana ya kumfanya awaamini watafanya kweli msimu ujao ili kushindana na Manchester City kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu ujao.

Toby amegoma kusaini mkataba mpya huko Spurs, lakini Willian anaripotiwa pia kutaka kwenda kufanya kazi na kocha wake wa zamani ambaye walikuwa wote Stamford Bridge na kupata mafanikio makubwa.

Sambamba na hilo, Mourinho ameripotiwa pia kuwa katika hatua za mwisho kabisa kumkamatia kiungo wa Kibrazili, Fred anayekipiga kwenye kikosi cha Shaktar Donetsk, kwenda kuchukua mikoba ya kiungo Michael Carrick, atakayehamia kwenye benchi la ufundi msimu ujao na Marouane Fellaini, ambaye anaripotiwa ataachana na maisha ya Old Trafford.Kuhusu Willian, Chelsea inasuasua juu ya kumwaachia kwa sababu imeona namna ilivyomuuzia Mourinho, kiungo Nemanja Matic mwaka jana na kwenda kucheza soka la kiwango cha juu sana huko Man United.