Modric atamani Croatia iinge kwa Real Madrid

Monday June 11 2018

 

By Fadhili Athumani

Moscow,Russia. Zikiwa zimesalia siku tatu tu kipute cha Kombe la Dunia, kianze kutimua vumbi, kiungo wa Real Madrid, Luca Modric ametoa ya moyoni.


Nyota huyo anayeongozwa kikosi cha Croatia kinachoelekea nchini Russia kwa ajili ya Kombe la Dunia, amesema anatamani angeweza kubadilisha mafanikio aliyopata katika klabu ya Real Madrid na Kombe la Dunia.


Modric, amekuwa sehemu ya kikosi cha Real ‘Los Blancos’ kilichoweka rekodi ya kutwaa kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu mfululizo kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano hayo, na sasa anatamani mafanikio hayo angeyapata na timu ya Croatia katika Kombe la Dunia.


Kiungo huyo, aliiongiza safu ya kiungo cha Madrid katika ushindi wa 3-1 walioupata dhidi ya Liverpool Jijini Kiev. Lakini Modric anasema kichapo walikitoa kwa Paris Saint-Germain, Juventus na Bayern Munich kilikuwa kitakatifu na hivyo anatamani kufanya hivyo kwenye fainali ya Kombe la dunia.


Akizungumza katika hafla ya tuzo ya wanasoka bora wa Croatia, Modric alisema: "Inaonekana hatuwezi kufanya kitu kizuri bila ya kuwa na Drama. Lakini safari hii, tulichokifanya kitabaki kuwa historia. Tuliwatoa mabingwa wa Ufaransa, Italia na Ujerumank kabla ya kuwavuruga Liverpool.


Modric (32), ambaye amefanikiwa kubeba mataji manne ya Ligi ya Mabingwa ulaya, La Liga moja na Copa del Rey mara moja tangu atue Santiago Bernabeu mwaka 2012, alisema kama ingekuwa uwezo wake, angebadilisha makombe kadhaa aliyoshinda na klabu take hiyo kwa ajili ya Kombe la Dunia.


"Namshukuru Mungu kwa mataji na mafanikio tuliyopata mpaka sasa. Kubeba Ligi ya Mabingwa ilikuwa ni ndoto ila sasa sio ndoto tena. Ndoto yangu ni kutwaa Kombe la Dunia. Ningekuwa na uwezo, ningetoa makombe kadhaa niloyotwaa na Real Madrid kwa ajili ya mafanikio ya Croatia kwenye Kombe la Dunia," alisema Modric.