MAKINI Pep Guardiola anakumbuka kila tukio baada ya mechi

Muktasari:

Pep naye alimhakikishia Thiago kuwa timu itafanya kila liwezekanalo ili kufikia fainali ya DFB Pokal na Ligi ya Mabingwa kwa ajili yake na Thiago akaahidi kupambana ili awe tayari kwa fainali zote hizo ingawa ukweli ni kwamba haikuwa rahisi kwa wote hao kufikia malengo hayo.

KATIKA toleo lililopita kwenye Pep Confidential, Mwandishi Marti Perarnau alizungumzia kuumwa kwa Thiago na matarajio ya mchezaji huyo kupona haraka huku Pep akimhakikishia watafanya kila linalowezekana kupata mafanikio. Sasa endelea…

Pep naye alimhakikishia Thiago kuwa timu itafanya kila liwezekanalo ili kufikia fainali ya DFB Pokal na Ligi ya Mabingwa kwa ajili yake na Thiago akaahidi kupambana ili awe tayari kwa fainali zote hizo ingawa ukweli ni kwamba haikuwa rahisi kwa wote hao kufikia malengo hayo.

Huyo ndiye Pep pale anapokuwa mwenye furaha baada ya mechi, mara tu anapomaliza kuzungumza na vyombo vya habari, Pep anakwenda kwa wachezaji wake kwenye mgahawa uliopo Allianz Arena, anapata mvinyo kidogo na vitafunwa kidogo vya haraka haraka na nusu saa inayofuata anaitumia kuizungumzia mechi.

Kwa kawaida huwa anasimama au kukaa katika moja ya meza lakini ingawa anakuwa hajala siku nzima lakini haonyeshi dalili zozote za kutaka kukimbilia chakula.

Katika hali ya kawaida mara baada ya mechi anakuwa ni mtu mwenye njaa lakini hawi katika utulivu wa kiakili wa kuwa tayari kuanza kula aina ya samaki anaowapenda.

Awali ya yote anapenda kutumia walau dakika 30 hivi kupunguza machovu na hasira si tu alizokuwa nazo katika mechi, bali kwa kipindi cha siku kadhaa. Kwa hiyo anajiweka katika hali ya utulivu na kuanza kuzungumzia karibu kila kitu kilichojitokeza katika mechi, kila kilicho katika fikra zake.

“Mliona alichokifanya Rafinha katika dakika ya 18? Alirudi nyuma mita kama mbili hivi na kuziba njia zote ambazo walikuwa wakizitumia kujipanga kwa ajili ya kutushambulia.

Hapana hakikuonekana chochote katika hilo. Pep amebarikiwa kumbukumbu kama zile za picha ambazo zinamfanya kukumbuka na kuanza kuchambua kila kitu kilichojitokeza katika mechi.

Katika hilo anakuwa kama mwenye kufanana na staa wa tenisi, Rafa Nadal ambaye anaweza kukumbuka kila mpira alioupiga katika mechi yake na alivyopata pointi, jinsi alivyotawala mchezo au makosa ambayo yeye au mpinzani wake ameyafanya na tukio lipi lilikuwa muhimu.

Na yote hayo yanaendelea kuwa katika fikra zake muda mrefu baada ya mechi kumalizika, ni hivyo hivyo kwa Pep, anakumbuka kila hatua ya mchezo, jinsi lilivyotokea, nini kilitokea baada ya tukio hilo, ni mchezaji yupi aliyehusika na nini matokeo ya tukio hilo.

Kwa upande mwingine katika yote hayo haweki mkazo au fikra zake kwenye rekodi.

“Hamkumiliki mpira kwa sana, ni asilimia 63 tu,’’ nilimwambia naye akajibu, “Ndio, hilo ni hakika, lakini ni Starke tu aliyeugusu mpira zaidi kwa upande wa wachezaji wa Hoffenheim kuliko mwingine yeyote.”

Suala la rekodi huwa halimsumbui Pep kinachomvutia zaidi ni mchezo wenyewe, na uchambuzi wa baada ya mechi, “Umeona jinsi Philip (Lahm) alivyokuwa makini? Uliona jinsi huyu jamaa alivyogeuka na kulinda umiliki wetu wa mpira na jinsi alivyowavuruga wapinzani.

Au unamsikia akisema, “natakiwa kuzungumza na Kroos kwa sababu katika mechi dhidi ya Manchester (United) hakuwa mwenye kujaribu kutawala kasi ya mchezo kama anavyofanya kwa kurudi kulia kwa sababu huwa wanamtabiria hilo na kumnyang’anya mpira kisha kufanya shambulizi la kushitukiza.”

Anamwita Planchart kwenye meza, “Carles (Planchart) kesho asubuhi nipe video inayohusisha tukio la dakika ya 36, kile kitu ulichonitajia nataka kumuonyesha beki wa kati namna nzuri ya kujipanga.”

Katika hii nusu saa inayovutia na ya kipekee, ambayo tumekaa kwenye kona ya mgahawa tukiguswa na hisia kama tuliochanganyikiwa kama vile ndio kwanza tuko katikati ya mechi inayoendele, hapo Pep anakuwa mwenye kugusa matukio yote ya kuvutia yaliyotokea kwenye mechi.

Anaichambua mechi vipande vipande kama daktari anayetibu mgonjwa mwenye kuhitaji operesheni, ni kama anakuwa na fuvu alilolichambua mishipa yote, hapo anakuwa mwenye kumfanyia tathmini kila mchezaji wake, kila hatua ya mchezo na kila tukio muhimu.

Atawafanyia tathmini timu pinzani, kila hatua ya mechi, kila tukio muhimu, ataendelea kuchambua namna mabao yalivyopatikana, hapo atagusia kwa uhakika bao lilipoanzia kutengenezwa hadi hatua ya mwisho ya mpira kuingia ndani ya nyavu.

Itaendelea Jumanne ijayo…