Kocha Spurs akili yote kwa Newcastle leo

Muktasari:

  • Pochettino amewashtukiza wachezaji wake walioziwakilisha nchi zao katika fainali za 21 za Kombe la Dunia zilizomalizika mwezi uliopita nchini Russia, licha ya kwamba hawajafanya mazoezi ya kutosha.

London, England. Kocha wa timu ya Tottenham, Mauricio Pochettino ameingiwa na kiwewe kuelekea mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu dhidi ya Newcastle United.

Pochettino amewashtukiza wachezaji wake walioziwakilisha nchi zao katika fainali za 21 za Kombe la Dunia zilizomalizika mwezi uliopita nchini Russia, licha ya kwamba hawajafanya mazoezi ya kutosha.

Wachezaji hao walikuwa wamepewa mapumziko lakini kutokana na kupata majeruhi wapya ameamua jana Ijumaa akabadili mawazo na kuamua kuwatumia wachezaji hao.

Kocha huyo amechanganyikiwa baada ya baadhi ya wachezaji kuongezeka katika orodha ya majeruhi kutoka mmoja hadi kufikia wane ambao ni Juan Foyth, Erik Lamela, Victor Wanyama na Harry Winks, ambao hawatakuwepo kwenye mechi za kwanza.

Kocha huyu ambaye ameandika historia ya kuwa kocha wa kwanza wa Ligi kuu England kutosajili mchezaji hata mmoja katika dirisha la usajili wa kiangazi tangu kuanzishwa kwake mwaka 2003.

Hilo limemfanya Pochettino kuamua kuwatumia wachezaji hao waliokuwa mapumzikoni kuanza katika mchezo ni pamoja na nahodha wa England, Harry Kane.

Kocha wa Newcastle United, Rafa Benitez yeye atamkosa mchezaji mmoja pekee aliye majeruhi Florian Lejeune, ambaye amefanyiwa upasuaji wa goti.

Mechi za Ligi Kuu England leo ni Newcastle dhidi ya Tottenham saa 8:30 mchana, Bournemouth itaialika Cardiff saa 11:00 jioni, Fulham dhidi ya Crystal Palace sa 11:00 jioni, Huddersfield watawakaribisha Chelsea saa 11:00 jioni, huku Watford       wakiwaalika Brighton na Wolves watakuwa wenyeji wa Everton saa 11:00 jioni.