Guardiola aitosa Argentina kweupe

Muktasari:

  • Guardiola amekuwa akitajwa kuwa anastahili kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Jorge Sampaoli aliyejiuluzu baada ya kushindwa kuivusha Argentina hatua ya 16 bora ya fainali za Kombe la Dunia.

Manchester, England. Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola ameikataa ofa ya kuinoa timu ya Taifa ya Argentina, akisema mengi yanayosemwa kuhusiana na suala hilo.

Guardiola amekuwa akitajwa kuwa anastahili kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Jorge Sampaoli aliyejiuluzu baada ya kushindwa kuivusha Argentina hatua ya 16 bora ya fainali za Kombe la Dunia.

Rais wa Chama cha soka Argentina, Claudio Tapia, alisema kutokana na kuondoka kwa Sampaoli chama hicho kimewateua Lionel Scaloni na Pablo Aimar, kuwa makocha wa muda wa timu ya Taifa.

“Ninasikitika kuona ninahusishwa na kuwa Kocha wa Argentina, bahati mbaya mimi sijazungumza na yeyote kati ya viongozi wa Chama cha soka, nashangaa mmoja kati ya viongozi amesema wanashindwa kunifuata kwa kuwa mimi nitahitaji fedha nyingi za mshahara tuseme wao wanajua mshahara ninaolipwa hapa?,” alihoji Guardiola.

Kocha huyo yupo katika mwaka wa tatu wa kuinoa Man City, akiwa tayari ameipa ubingwa wa Ligi Kuu England na kuifikisha katika robo fainali ya Ligi ya mabingwa Ulaya ambayo ni hatua ya juu kabisa kufikia na timu hiyo.

Baada ya kuhisi watashindwa kumpata Guardiola, Tapia amewaorodhesha makocha wa kujadiliana nao kuhusu kupewa jukumu hilo kuwa ni Kocha wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino, yule wa Atletico Madrid, Diego Simeone na kocha wa River Plate, Marcelo Gallardo ili mmoja wao amrithi Sampaoli, atakayepewa kazi hiyo atatangazwa Desemba mwaka huu.