For sale !

Muktasari:

Juzi Pogba alicheza vema katika pambano dhidi ya Bournemouth akipika bao moja la Romelu Lukaku katika ushindi wa mabao 2-0, lakini Scholes anadai kiwango ambacho Pogba alionyesha dhidi ya West Brom kinaweza kumtia sokoni mwishoni mwa msimu.

KAMA unayaamini maneno ya wahenga basi unaweza kumuamini Paul Scholes. Anadai Kocha Jose Mourinho sio mtu wa mchezomchezo na anaweza kumuweka sokoni wajina wake, Paul Pogba mwishoni mwa msimu huu.

Juzi Pogba alicheza vema katika pambano dhidi ya Bournemouth akipika bao moja la Romelu Lukaku katika ushindi wa mabao 2-0, lakini Scholes anadai kiwango ambacho Pogba alionyesha dhidi ya West Brom kinaweza kumtia sokoni mwishoni mwa msimu.

Scholes, mmoja kati ya wakongwe wanaoheshimika Old Trafford amedia Pogba alionyesha kiwango cha chini katika mechi hiyo ya Jumapili ambayo United ilichapwa bao 1-0 na West Brom ambayo inashika mkia katika ligi hiyo.

Vibonde hao walimiliki dimba na kumfunika Pogba na kiwango chake kiliendelea kumchonganisha na Kocha Mourinho ambaye katika siku za karibuni amekuwa hana maelewano na staa huyo mrefu wa kimataifa wa Ufaransa.

“Nadhani anaweza kuondoka. Sijui, siongei na mtu yeyote wa ndani ya klabu. Lakini ukiangalia mambo kwa nje uhusiano wao hauonekani kuwa mzuri kabisa. Ukitazama kiwango cha mechi ya Jumapili (Dhidi ya West Brom) ni kama vile anasema ‘Sina mpango na kocha anachofikiria, sijali anachofikiria kuhusu mechi ya leo. Sitamsikiliza kwa chochote, naenda tu kucheza kwa jinsi ninavyojisikia,” alichonganisha Scholes.

“Na nadhani huo ni ukosefu wa heshima kwa kocha na wachezaji wenzake,” aliongeza Scholes ambaye kwa sasa amegeukia kazi ya uchambuzi.

Hiyo sio mara ya kwanza kwa Pogba kukosolewa vikali na Scholes ambaye katika siku za karibuni alidai staa huyo haonekani kuwa fiti na hathibitishi uhalali wa kununuliwa kwa dau kubwa la Pauni 89 milioni.

Januari mwaka huu, Mourinho wakati akiwa katika uhusiano mzuri na Pogba alidai Scholes alikuwa anamuonea wivu tu Pogba kwa sababu alikuwa analipwa pesa nyingi huku akidai Scholes alikuwa mchezaji mzuri sana lakini sio mchambuzi mzuri.

Kwa sasa kibao kimegeuka na Mourinho anaweza kuungana na Scholes baada ya siku za karibuni kuanza kumtumia Pogba kwa minyato zaidi tofauti na ilivyokuwa awali na kuna nyakati ambazo amekuwa akimsugulisha benchi katika mechi muhimu kama ilivyokuwa katika pambano la Ligi ya Mabingwa dhidi ya Sevilla ugenini.

Mourinho pia amemuita benchi Pogba katika mechi dhidi ya Tottenham, Newcastle na juzi dhidi ya Bournemouth ambapo mchezaji huyo alikataa kutoa mkono wake kwa kocha huyo mara alipotolewa nje. Baadaye alielekea katika vyumba vya kubadilishia nguo kabla ya kuamua kurudi uwanjani.

Kumekuwa na madai mbalimbali kwamba Mourinho ameshindwa kumtumia vema staa huyo wa zamani wa Juventus ambaye anaonekana kuwa mchezaji anayemudu zaidi katika staili ya kushambulia kuliko staili ya kujihami ambayo ni maarufu kwa Mourinho.

Tayari wakala wa staa huyo, Mino Raiola anadaiwa kumuweka sokoni mteja wake ambapo tayari anadaiwa kupiga simu katika klabu za Manchester City, Real Madrid na PSG ambazo zina uwezo wa kipesa wa kumnunua staa huyo.

Wiki mbili zilizopita Kocha wa City, Pep Guardiola alitoa madai kwamba walipewa fursa na Raiola kumnunua Pogba katika dirisha la Januari lakini hawakuwa na mpango huo kwa sababu wanaamini staa huyo ni ghali.

Mourinho alidai kulikuwa na mtu mmoja alikuwa anasema uongo kati ya Guardiola au Raiola kuhusu suala hilo.