Dili la Ramsey lakwama tena

Muktasari:

Arsenal walikuwa kwenye hatua nzuri ya kumsainisha mkataba wa miaka mitano kiungo huyo, lakini mambo yamegeuka na mpango mzima kukwama baada ya kuwapo na shida kuhusu Ivan Gazidis.

ARSENAL imeripotiwa kukwama kwenye kukamilisha mazungumzo yake ya kumpa mkataba mpya kiungo wao matata kabisa, Aaron Ramsey.

Arsenal walikuwa kwenye hatua nzuri ya kumsainisha mkataba wa miaka mitano kiungo huyo, lakini mambo yamegeuka na mpango mzima kukwama baada ya kuwapo na shida kuhusu Ivan Gazidis.

Ramsey ameripotiwa alishakubali kusaini mkataba mpya wenye thamani ya Pauni 250,000 kwa wiki ili aendelee kutoa huduma yake Emirates, lakini mambo yameanza upya kutokana na shida kidogo iliyojitokeza kwenye mpango huo.

Mkurugenzi Mtendaji Mkuu, Gazidis, ndiye aliyekuwa akifuatilia jambo hilo kulikamilisha, lakini yeye mwenyewe ameibua wasiwasi mkubwa kutokana na kuwapo kwa ripoti yupo kwenye mipango ya kuachana na wakali hao wa Ligi Kuu England.

Huko Italia kumekuwa na ripoti kwamba Gazidis amepanga kwenda kujiunga na moja ya vigogo wa Serie A jambo linalozua hofu kubwa huko Emirates kutokana na umuhimu wa bosi huyo kwenye kikosi hicho cha Arsenal.