Conte akibaki, mastaa hawa wanaondoka

CHELSEA mambo ni moto. Ishu ya Antonio Conte inaonekana kuwakalia kooni.

Unajua ishu ikoje? Ni hivi, kuna wachezaji watatu mastaa wakubwa kwenye kikosi hicho huko Stamford Bridge wameripotiwa kuwa, watabeba mabegi yao na kuondoka kama Conte ataendelea kuwa kocha wa timu hiyo msimu ujao.

Ripoti za kutoka Stamford Bridge zinadai Conte ametibuana na baadhi ya wachezaji muhimu kwenye kikosi hicho katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.

Kwa hali ya mambo ilivyo ni kama Conte atabaki kwenye timu, basi Chelsea itakuwa kwenye hatari ya kuwapoteza wachezaji watatu muhimu kabisa ambao wamekuwa na msaada mkubwa kwenye kikosi.

Wachezaji hao wanaotajwa ni Eden Hazard, David Luiz na Willian, ambao wameripotiwa kuanza kutafuta mlango wa kutokea kama Mtaliano huyo ataendelea kubaki kwenye kikosi hicho.

Chelsea kwa sasa haitaki kumwachia Conte kwa haraka kwa sababu jambo hilo litaifanya imlipe fidia ya Pauni 9 milioni ambazo ni nyingi.

Kocha wa zamani wa Napoli, Maurizio Sarri, ndiye anayepewa nafasi ya kwenda kuchukua mikoba ya Conte huko Stamford Bridge kama ataondoka klabuni hapo.