Mane anavyofukuzia rekodi za Waafrika Mabingwa UlayaMane anavyofukuzia rekodi za Waafrika Mabingwa Ulaya

Muktasari:

  • Kitendo cha kucheza tu kwenye mechi hiyo, supastaa Sadio Mane alitengeneza rekodi ya kuwa mchezaji wa Afrika wa 20 kucheza kwenye fainali ya michuano hiyo mikubwa kabisa kwa ngazi za klabu Ulaya.

MAKUNDI ya Ligi ya Mabingwa Ulaya yameshapangwa na mchakamchaka wa michuano hiyo utaanza rasmi Septemba 18, mwaka huu. Kwenye fainali iliyopita, iliyofanyika Mei 26, Liverpool ilichapwa na Real Madrid 3-1, huku bao la kujifariji la wababe hao wa Anfield likifungwa na Msenegali, Sadio Mane.

Kitendo cha kucheza tu kwenye mechi hiyo, supastaa Sadio Mane alitengeneza rekodi ya kuwa mchezaji wa Afrika wa 20 kucheza kwenye fainali ya michuano hiyo mikubwa kabisa kwa ngazi za klabu Ulaya.

Hiyo ina maana Waafrika hawapo nyuma katika kuonyesha makali yao katika mikikimikiki hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na hii hapa ni orodha ya mastaa wa Afrika waliocheza mechi nyingi katika michuano hiyo.

5. Samuel Kuffour- Mechi 73

Kwenye soka la klabu za Ulaya, Kuffour alizichezea klabu za Bayern Munich, AS Roma na Livorno.

Kuhusu Ligi ya Mabingwa Ulaya kitu kinachokumbukwa zaidi kuhusu yeye ni kitendo chake cha kumwaga machozi uwanjani wakati kikosi chake cha Bayern Munich kilipochapwa kwa mabao ya dakika za majeruhi katika fainali msimu wa 1998/99. Bayern ilichapwa 2-1 na Manchester United.

Lakini Kuffour alikuja kufarijika kwa ubingwa msimu wa 2000/01, alipoisaidia Bayern kuichapa Valencia kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 1-1. Kwa jumla beki huyo wa Ghana amecheza mechi 73.

4. Kolo Toure- Mechi 74

Beki wa kati, Muivory Coast, Kolo Toure ametamba kwenye soka la Ulaya akipiga kwenye klabu za Arsenal, Manchester City, Liverpool na Celtic.

Mwaka jana staa huyo alitangaza kustaafu na hivyo kuhamia kwenye benchi la ufundi la timu ya Celtic. Lakini, ubora wake wa ndani ya uwanja umemfanya awe mmoja kati ya wachezaji wa Kiafrika waliocheza mechi nyingi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuonekana uwanjani kwenye mechi 74 za michuano hiyo.

3. Michael Essien- Mechi 76

Akiwa kwenye ubora wake kiungo, Michael Essien alikuwa mtamu kwelikweli uwanjani. Umahiri wake wa kulisukuma gozi ulianza kuonekana tangu enzi akiwa na Lyon, kabla ya kunaswa na Chelsea, ambako aliendelea kutamba kisha kwenda Real Madrid na AC Milan.

Kwenye ubora wake hakuna kocha ambaye angethubutu kumweka benchi Essien hasa zinapokuja mechi muhimu na ndiyo maana ameonekana uwanjani akikipiga kwenye mechi 76 za Ligi ya Mabingwa Ulaya. Essien alibeba taji hilo la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2012 wakati Chelsea ilipoichapa Bayern Munich kwa penalti.

2.Samuel Eto’o- Mechi 82

Mwaka 2010, straika Mcamerooni, Samuel Eto’o alikuwa mchezaji wa kwanza kubeba mataji matatu makubwa kwa msimu mmoja mara mbili mfululizo, akitokea kufanya hivyo huko Barcelona kisha kwenda kurudia Inter Milan.

Aliweka tena rekodi ya kuwa mchezaji wa pili kwenye historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kufunga kwenye fainali mbili mfululizo za Ligi ya Mabingwa Ulaya na alikuwa mchezaji wa nne baada ya Marcel Desailly, Paulo Sousa na Gerard Pique, kushinda taji hilo la Ulaya miaka miwili mfululizo wakiwa na timu mbili tofauti.

Huko Ulaya, Eto’o amepita kwenye timu nyingi ikiwamo Real Madrid, Mallorca, Barcelona, Inter, Chelsea na Everton, lakini kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya amecheza mechi 82.

1.Didier Drogba- Mechi 94

Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kitu ambacho kimebaki kwenye kumbukumbu ya kudumu kuhusu mshambuliaji Didier Drogba ni ile fainali ya mwaka 2012, aliisaidia Chelsea kuichapa Bayern Munich na kubeba ubingwa.

Kwanza Drogba aliyecheza mechi 94 Ulaya, alipiga bao la kusawazisha katika dakika ya 88 kabla ya kupiga penalti ya ushindi na hivyo kuwafanya The Blues kubeba ubingwa wao wa kwanza wa michuano hiyo. Kwenye soka la Ulaya, Drogba amepita kwenye timu nyingi, lakini mahali ambako alicheza kiushindani zaidi ni Marseille, Chelsea na Galatasaray.