Chama la England litakaloanza hili hapa

ENGLAND bana, kweli wana kiherehere. Kombe la Dunia linaanza wiki ijayo huko, lakini wao tayari wameshaweka hadharani kikosi chao kitakachoanza kwenye mechi ya kwanza na Marcus Rashford ataanzia benchi licha ya kuonyesha kiwango kikubwa kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Costa Rica, Alhamisi iliyopita.

Kwenye kikosi hicho cha kwanza kitakachomenyana na Tunisia, Jordan Henderson ataanza akicheza kiungo ya kukaba mbele ya mabeki watatu wa kati na hivyo Eric Dier ataanzia kwenye benchi.

Danny Rose amepata nafasi ya kuanza pia mbele ya Ashley Young na Kocha Gareth Southgate ameamua kumtumia Raheem Sterling nyuma ya mshambuliaji wa kati, nahodha Harry Kane.

Kocha Southgate amesema ameamua kumwanzisha Rose baada ya kukoshwa na kiwango chake katika mechi zilizopita licha ya staa huyo wa Tottenham Hotspur kutokea kwenye maumivu makali ya goti miezi 16 iliyopita. Kikosi hicho kilivyo, mabeki wa kati watatu ni Harry Maguire, John Stones na Kyle Walker, huku wachezaji wengine walioanza kikosini ni Trippier, Jesse Lingard na Dele Alli.

England imekuwa na uhakika wa kwenda kufanya vyema huko Russia baada ya kuruhusu bao moja tu ndani ya mchezo wa kawaida katika mechi sita za kirafiki.