YES! Arsenal bado kidogo tu kwa Sokratis

ARSENAL imeripotiwa kuwa kwenye hatua za mwisho kabisa kukamilisha dili la kumnasa beki wa kati wa Borussia Dortmund, Sokratis Papastathopoulos huku dili hili likiwagharimu Pauni 16 milioni.

Kumekuwa na ripoti Arsenal imekubali kulipa kiasi hicho cha pesa kwa ajili ya kuongeza beki mwingine kwenye kikosi chao baada ya kumnasa mmoja kutoka Juventus.

Mgiriki huyo atakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa na Kocha Unai Emery baada ya kumnyakua beki mwingine, Stephan Lichsteiner kutoka Juventus ya Italia.

Sokratis amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake huko Dortmund na kinachoelezwa, atasaini mkataba wa miaka mitatu na wababe hao wa Emirates.

Emery amedaiwa anataka kusajili mabeki wenye uzoefu baada ya Per Mertesacker kustaafu huku Laurent Koscielny akitarajiwa kukosa mechi kibao za mwanzo wa msimu ujao. Sokratis amekuwa kwenye kikosi cha Dortmund kwa miaka mitano baada ya kujiunga hapo akitokea Werder Bremen mwaka 2013.