Matic awaambia mabosi, mpeni pesa Mourinho alete majembe

Muktasari:

Kiungo Matic alisema hilo baada ya kushuhudia kikosi chake cha Man United kikipigwa bao 1-0 na timu yake ya zamani Chelsea kwenye fainali ya Kombe la FA huko Wembley juzi Jumamosi na hivyo kupoteza nafasi ya kubeba taji msimu huu.

KIUNGO wa Manchester United, Nemanja Matic amewaambia mabosi wa timu hiyo kuhakikisha wanampa pesa Kocha Jose Mourinho ili kufanya usajili wa maana watakaokuja kuifanya timu hiyo kuwa matata uwanjani.

Kiungo Matic alisema hilo baada ya kushuhudia kikosi chake cha Man United kikipigwa bao 1-0 na timu yake ya zamani Chelsea kwenye fainali ya Kombe la FA huko Wembley juzi Jumamosi na hivyo kupoteza nafasi ya kubeba taji msimu huu.

Katika mchezo huo, Mourinho alianza na makinda wa Kiingereza, Jesse Lingard na Marcus Rashford, ambao viwango vyao vya kiuchezaji vimekuwa vikipanda na kushuka kama homa za vipindi, huku kocha mwenyewe akidai straika wake Romelu Lukaku, alijitangaza kwamba hayupo fiti kucheza mechi hiyo.

“Tunahitaji wachezaji wengine wachache kwenye kikosi na baada ya hapo ndipo tutaweza kupigania ubingwa na naamini hilo litafanyika,” alisema Matic.

Hata hivyo, Matic, bado haamini kama Man United imeachwa mbali sana kiubora na wapinzani wao kutokana na namna walivyocheza kwenye fainali hiyo ambapo walifungwa kizembe.

“Tulifanya kosa moja lililosababisha bao, lakini upande mwingine tulicheza soka maridadi kwa dakika zote 90,” alisema Matic na kuongeza: “Ninadhani tulistahili kitu zaidi, lakini hivi ndivyo soka ilivyo, kosa moja unaadhibiwa na wakati mwingine unapoteza kabisa mechi na hilo ndilo lililotutokea. Nimefurahi kwa namna timu ilivyocheza, imani ni wakati mwingine bahati itakuwa upande wetu.”